Mahakama ya Rufani nchini imetupilia mbali pingamizi dhidi ya maombi ya Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, Marehemu Reginald Mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi yaliyohusu wosia alioacha Mengi.
Jacqueline amefungua maombi ya mapitio ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 18, 2021 na Jaji Yose Mlyambina iliyobatilisha wosia uliokuwa unadaiwa kuandikwa na marehemu Mengi wakati wa uhai wake, ambapo anaiomba Mahakama ya Rufani ifanye mapitio ya hukumu hiyo na hatimaye ibadilishe.
Kufuatia maombi hayo wajibu maombi wa kwanza Abdiel Reginald Mengi, ambaye ni mtoto wa marehemu Mengi wa mke mkubwa na Benjamin Abraham Mengi (mdogo wake na marehemu Mengi) walimwekea Jacqueline pingamizi la awali la hoja za kisheria wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali maombi yake bila kuyasikiliza.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake (kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi) imetupilia mbali hoja zote za pingamizi dhidi ya maombi hayo ya Jacqueline na badala yake imekubali kuyasikiliza maombi hayo.