Bunge la Kisiwa cha Barbados limemchagua Bi. Dame Sandra Mason (72) kwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo na pia Rais wa kwanza Mwanamke baada ya kumuondoa Malkia Elizabeth wa Uingereza kuwa kiongozi mkuu wa Taifa hilo.
Bi. Dame Sandra Mason ataapishwa kuwa Rais wa Taifa hilo Novemba 30, 2021 siku ambayo kisiwa hicho kitaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wake kutoka kwa Uingereza.
Mwaka 2019 kisiwa cha Barbados kilitangaza kumvua madaraka Malkia Elizabeth na kuifanya nchi hiyo kuwa Jamhuri, ambapo Waziri Mkuu wa Kisiwa hicho, Mia Mottley alisema, “Muda umefika sasa kuachana na ukoloni na mambo yote tuache nyuma na kusoma mbele.”
Baada ya kauli ya Waziri huyo, ngome ya Kifalme ya Buckingham Uingereza ilitoa tamko kwamba, jambo hilo ni kati ya Serikali pamoja na watu Barbados, na pia ni jambo ambalo wamekuwa wakilijadili kwa muda mrefu sana.
Barbados ni kisiwa chenye watu 285,000, na ni moja ya kisiwa chenye idadi kubwa ya watu kwa visiwa vya Karibiani. Barbados sio kisiwa cha kwanza kujitoa kwenye utawala wa chini ya Uingereza, bali pia Guyana ilijitoa mwaka 1970 miaka minne tu baada ya kupata Uhuru kutoka kwa Uingereza.
Kwa upande wa Tanzania ilikuwa Jamhuri mwaka 1962 mwaka mmoja baada ya kupata Uhuru kutoka kwa Uingereza.
Visiwa vya Trinidad na Tobago walijitoa 1976 na visiwa vya Dominica kikafuta 1978.
Nchi ambazo zimepata uhuru lakini bado kiongozi wake wa nchi ni Malkia Elizabeth wa Uingereza ni, Bahamas, Belize, Jamaica, ST Kitts & Nevis, Antigua & Barbuda, St Lucia, Grenada, St. Vicent & The Grenadines, Papua New Guinea, Solomon Islands, Tuvalu, New Zealand, Australia pamoja na Canada.