Kwa kipindi kirefu bara la Afrika limejulikana kama bara la njaa na kuupa ukweli kwamba kwa miaka dahari, kabla ya kuja kwa wakoloni barani Afrika kulishakuwa na mifumo ya uzalishaji na utunzaji wa chakula ambayo ni ya kipekee na haikuwahi kuwapo sehemu yeyote ile duniani.
Watumwa waliposafirishwa kutoka Afrika kuenda Bara la Ulaya, Visiwa vya Karibiani pamoja na Amerika, waliondoka na ujuzi wao katika sanaa ya upishi, utunzaji wa chakula pamoja na uzalishaji. Sanaa hiyo iliwafanya waweze kujitegemea na kuendelea kuishi wakati wakipitia dhoruba wakati wa biashara ya utumwa.
- Mchele/Wali
Mbegu ya kwanza kabisa ya Mchele nchini Marekani ilifika 1685 kutoka visiwa vya Madagascar. Katika jimbo la Carolina nchini Marekani ndipo kulianzishwa jaluba nyingi za mashamba ya mpunga. Wazungu wa Marekani hawakuwa na utaalamu wa kutosha katika kudhatiti kilimo hicho, ndipo walitumia watumwa kutoka Afrika ya Magharibi waliokuwa wajuvi kwenye kilimo hicho.
- Kahawa
Wengi hunasibisha asali ya zao la kahawa na Amerika ya Kusini pamoja na Amerika ya Kati, lakini ukweli ni kwamba ardhi ya zamani ya Malkia wa Sheba, Ethiopia, ndio uzao wa zao la Kahawa. Neno la lenyewe ‘Coffee’ litumikalo kwenye lugha ya kingereza, limetoholewe kutoka mji uitwao Kaffa huko Ethiopia ambapo ndipo asili ya zao la kahawa Duniani. Hadi wazungu wanatia nanga kwenye pwani za Ethiopia karne ya 16, tayari Ethiopia ilishabobea kwenye uchakati, upandaji, usindikaji pamoja na biashara ya zao hilo.
- Viazi Vitamu
Viazi vitamu ndio kilikuwa chakula kikuu cha watumwa, zao hili huweza kuliwa hata bila kupikwa mara nyingine kutoka na kadhaa yake ya sukari asilia. Wakati biashara ya utumwa imeanza kushamiri mwanzoni mwa karne ya 16, wafanyabiashara hiyo haramu kwa umoja wao waliingia maazimo kwamba, meli ya watumwa ikibeba watumwa 500, basi ibebe na viazi vitamu 100,000 kama chakula cha watumwa wawapo safarini. Kwa njia hiyo viazi vilifika Amerika pamoja na Ulaya.
- Njugumawe
Njugumawe ni moja ya zao pia lenye historia ya utumwa kwenye kuwasilishwa kwake Ulaya na Amerika. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali njugumawe zilifika Florida nchini Amerika mwaka 1700 na zilifikishwa Carolina ya Kaskazini mwaka 1730 na hatimaye kuwa chakula kikubwa na pendwa huko Virginia. Njugu mawe zilikuwa msaada mkubwa sana baada ya vita vya Mapinduzi Marekani, kwani hukuwa haraka na hazidhuriwa na magugu, hivyo husaidia mifugo pamoja na binadamu kupata chakula cha haraka.
- Bamia
Bamia asili yake ni Ethiopia, na hadi leo hupandwa na kupendwa zaidi katika mataifa jirani na Ethiopia kama Eritea na Sudani. Wakati mavuno ya kahawa nchini Ethiopia yamekamilika, Bamia lilitumika kupandwa katika mashamba ya kahawa kwa ajili ya kurudisha rotuba katika mashamba ya kahawa na pia kutunza unyevunyevu shambani. Majani ya Bamia yalitumika kama dawa. Mwaka 1748 Bamia ilifikishwa Marekani na kupandwa Philadelphia.
- Tikiti Maji
Wanahistoria katika sekta ya vyakula bado wanakanganyana juu ya asili ya tunda hili, lakini wote husadiki kuwa kabla ya tikiti hili tulilalo leo, lilishakuwepo tikiti lenye ladha ya ugwadu huko Sudani na Misri ya kale. Miaka 2000 iliyopita, Mafarao wa Misri walilima zao hili, na lilitumika pia kwenye matambiko hasa ya maziko. Tikiti lilizikwa pamoja na maiti wakiamini kwamba litakuwa msaada wa maji kaburini kwa mpendwa wao pindi akisubiri siku ya kufufuliwa tena. Halikadhalika, tikiti liliwasilishwa Amerika na Ulay wakati wa Biashara ya Utumwa.