Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amesema Januari mwakani atapeleka taarifa ya utendaji wa Wakurugenzi wa halmashauri kwa mamlaka ya uteuzi. Waziri Ummy amesema Wakurugenzi wa Halmashauri wako kwenye kipindi cha miezi Sita ya uangalizi na kwamba taarifa ya utendaji kazi kwa robo ya pili itampa nafasi ya kutambua utendaji wao.
“Hii ni taarifa yao ya kwanza, tunasubiri taarifa ya pili baada ya hapo tutapeleka taarifa kwa Mheshimiwa Rais, Mkurugenzi gani anamudu kasi ya Rais nani aanamudu na kukidhi dhamira ya Rais Samia ya kutatua kero za Wananchi. Sitishii ndio ukweli siwezi kumthibitisha Mkurugenzi wakati utendaji wako hauridhishi.”
> BoT yaanzisha vita na wanaotumia noti vibaya
Waziri Ummy alisema moja ya vigezo vya upimaji kwa Wakurugenzi ni ukusanyaji wa mapato kulingana na makisio ya Halmashauri husika na kupeleka fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo pamoja na kutoa asilimia 10 ya mapato ya ndani kukopesha vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo alitolea mfano halmashauri ya Simanjiro inapeleka asilimia moja ya mapato ya ndani, yaani katika miezi 3 wamekusanya mapato ya shilingi milioni 700 na alipaswa kuelekeza shilingi milioni 280 kwenye miradi ya maendeleo ya kutatua kero za Simajiro iwe maji, afya au elimu lakini wamepeleka shilingi milioni 2.25.