Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, ametishia kujiiuzulu nafasi hiyo kwa madai ya kutokuheshimiwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Nice Munissy.
Mwenyekiti huyo alitoa malalamiko hayo kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mboje amesema tangu Mkurugenzi huyo mpya aanze kazi Wilayani hapo, kumekuwa hakuna tena kuheshimiana wala maelewano mazuri.
“Tangu mwaka 2011 nipoi kwenye Halmashauri hii, Wakurugenzi wote waliopita walikua wakiniheshimu lakini sasa hivi hakuna heshima ni bora nikachukua uamuzi wa kuachia ngazi ya Uenyekiti nibaki na udiwani wangu kutumikia wananchi”.
Mboje amesema kuna uwezekano wa changamoto kubwa zaidi kutokea kwenye Halmashauri yao kwani kuna shida nyingi sana na watumishi wa Halmashuri hiyo hawana maelewano mazuri akiongeza pia kwamba Mkurugenzi Munissy alimyima gari kwa ajili ya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amemtaka Mboje kutokua mnyonge bali kama kuna tatizo amuite Mkurugenzi wake wamalize changamoto hizo na ikishindikana wapeleke suala hilo katika kamati ya siasa ya CCM ili wasuluhishwe.