Chunusi ni uvimbe mdogo au kipele kidogo kwenye ngozi ambacho husababishwa na kuganda na mlundikano wa mafuta. Chunusi hutokea katika umri wowote ule, lakini mara nyingi hutokea wakati wa baleghe kwa wanaume na wanawake.
Mara nyingine chunusi huwa na maumivu makali na kusababisha usumbufu kwa mtu. Chunusi pia zinaweza kumpa mtu muonekana usiovutia au zinaweza kumfanya mtu kutojiamini kutokana na hali hiyo.
Chunusi ikionesha kuiva wengi huzitumbua au huagiza mtu amtumbue. Lakini yapo madhara yatokanayo na kuzitumbua chunusi zetu kwa mikono yetu. Utumbuaji wa chunusi unaweza kukuletea madhara yafuatayo.
1. Makovu kwenye ngozi
Haishauriwi kutumbua chunusi kwani inaweza kukusababishia makovu kwenye sura yako. Chunusi nyingine hutoa damu nyingi baada ya kutumbuliwa, hii ni dalili kuwa chunusi hiyo kuna uwezekano mkubwa ikaacha kovu. Ni vyema kuicha chunusi itumbuke yenyewe ukabaki na kazi ya kusafisha pekee.
2. Kusambaza bacteria
Kutumbua chunusi kwa mikono kunaweza kusababisha bakteria kusambaa kwenye maeneo mengine ya usoni kutoka kwenye chunusi iliyotumbuliwa.
3. Kuchelewa kupona
Chunusi kama itatumbuliwa inaweza kuharibu utaratibu wa asili wa kupona kwake, kwa kawaida chunusi hupona ndani ya siku 3 hadi 7 kama itaiva na kutumbuka yenyewe, lakini kama utachukua hatua mikononi mwako kuitumbua basi inaweza kuchukua hadi siku 14 kupona kabisa.
4. Uvimbe
Chunusi iliyowahishwa kutumbuliwa inaweza kukusababishia uvimbe usoni hivyo kukuondolea muonekano mzuri.
Kama unataka kutumbua chunusi zako, basi hakuna tatizo unaweza kufanya kwa njia sahihi.
1. Kabla hujatumbua chunusi hakikisha imetengeneza weupe kwa ndani, kabla ya kuwa na weupe maana yake ni kwamba chunusi hiyo haijaiva bado na kuitumbua ni kusababisha madhara
2. Osha mikono yako mara kwa mara ili usisambaze bakteria sehemu nyingine za mwili
3. Tumia dawa kama vile salicylic acid au benzoyl peroxide baada ya kutumbua kuondoa au kupunguza makovu
4. Tumia sindano pini au kitu chenye ncha kali kilichotibiwa. Zipo dawa maalumu kama spirit au sanitizer ambazo unaweza kutibu kifaa chako kabla ya kutumbua chunusi
5. Baada ya kuitumbua chunusi yako, hakikisha unapaka spirit au sanitizer kwenye kidonda cha chunusi kuzuia bakteria kusambaa zaidi.
Namna gani unaweza kuzuia chunusi zisikutoke?
1. Fanya mazoezi mara kwa mara kupunguza mafuta mwilini
2. Kunywa maji mengi
3. Osha uso wako kila ukitaka kulala, osha vizuri
4. Muone daktari wa ngozi wa maelezo ya kitaalamu zaidi.