Jeshi la Polisi nchi Tanzania leo November 30 limetoa taarifa kufuatia kuwepo kwa taarifa mbaya kuhusu jeshi hilo, Mnamo Novemba 29 mwaka huu kuna taarifa iliyonekeana kwenye gazeti ikisema “Askari wageuza simu za wizi mradi binafsi” huku leo kwenye chapisho lake la Novemba 30 liliandika kuwa “Mapya yaibuka askari kugeuza simu za wizi mradi binafsi”.
Kwenye taarifa iliyotolewa leo na Jeshi la Polisi kwa waandishi wa habari walikubali kupokea taarifa hizo kuanzia jana na kuanza kuifanyia uchunguzi, Katika uchunguzi huo wamebaini baadhi ya askari ambao sio waaminifu wanaofanya vitendo hivyo sambamba na hilo Jeshi la Polisi limetoa maelekezo kuhusu jinsi ambavyo wananchi wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu upotevu wa simu zao.
Jeshi la Polisi limesema kuwa sio kila askari polisi au kila kitengo kinashughulikia kesi za wizi wa simu, hivyo ikitokea mtu ameibiwa simu basi anatakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wakuu wapelelezi wa Wilaya (OC-CIDs), Wakuu wapelelezi wa Mkoa (RCOs) na Makamanda wa Polisi wa Mikoa (RPCs) kwani viongozi hao ndio wanahusika na kusimamia watu wanaoshughulikia simu zilizopotea.
Pia limetoa wito kwa wananchi waliotozwa fedha kutoa taarifa kwa viongozi hao kwani tayari wameshapewa maelekezo kuhusu hatua gani za kuchukua kwa askari waliofanya utovu wa nidhamu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limesema Vitendo vya askari hao kudai pesa ni tabia ya mtu binafsi na sio Jeshi la Polisi kwani jukumu lao ni kulinda maisha ya watu na mali zao.