Mwezi wa 12 (Desemba) ni mwezi unaombatana na sikukuu na mapumziko. Sikukuu za ‘Christmas’ na kuukaribisha mwaka unaofuata, hutawala zaidi mawazo ya wengi katika mwezi huu, lakini pia wengi hupata likizo kazini au kuamua kufanya safari na mambo mengine kwa ajili ya kufunga mwaka.
Kutokana na mambo hayo mengi, Desemba inaweza kuambatana na matumizi makubwa ya fedha iwapo mtu hatakuwa makini, hivyo ni vyema kuwa makini na kujitahidi kuepuka makosa ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kuyafanya.
Click Habari inakushauri kuzingatia mambo yafuatayo
1. Usiingie kwenye mtego wa ‘Sale’
Katika mwezi huu, maduka mengi yanapambwa na matangazo ya ‘Sale’ ikimaanisha kwamba wanatoa punguzo ya bei za bidhaa mbalimbali. Utakapoingia katika mtego huu, unaweza kujikuta umenunua vitu vingi usivyovihitaji kwa wakati huu, utakuwa umeburuzwa na nguvu ya soko.
Hakikisha unafahamu unachotaka kununua, nunua kwa sababu umetaka kununua na sio kwa sababu ya kuvutiwa na matangazo ya punguzo la bei.
2. Panga bajeti
Usichukulie poa matumizi ya Desemba, kuna vitu vingi vinaweza kuongezeka katika bajeti yako ya kawaida.
Hivyo ni muhimu kuwa walau na makadirio ya juu ya matumizi yako, na kupanga vizuri matumizi yako kwa kuangalia kipato chako.
3. Kumbuka kuwa kuna maisha baada ya Desemba
Baada ya Desemba utakuja mwezi Januari ambao kwa wengi pia unakuwa na matumizi mengi. Desemba inaweza kuwa ya sherehe lakini Januari ni ‘maisha baada ya sherehe’ ambayo huambatana na matumizi mengine ya msingi kama malipo ya ada za shule, sare na mahitaji mengine.
Hivyo unapotumia fedha zako mwezi huu, kumbuka kuhusu Januari na uhifadhi fedha kwa ajili ya mwezi huo na majukumu yake.
4. Usinunue zawadi za gharama kubwa
Usiingie katika mtego wa kuamini kwamba ni lazima ununue zawadi nyingi ili ukamilishe furaha yako na ile ya wale uwapendao. Usijiminye sana kwa sababu ya shamrashamra za Desemba.
Ni jambo jema sana kununua zawadi kwa ajili ya wale upendao lakini ‘usijaribu kujikuna ambapo mkono wako haufikii’.
5. Epuka ‘mitoko’ isiyo ya lazima
Moja kati ya mambo yanayoweza kukufanya utumie fedha nyingi nje ya bajeti, ni mizunguko (mitoko). Kila unapotoka sehemu moja kwenda nyingine unaongeza matumizi.
Jitahidi sana kuwa na ‘mitoko’michache.