Jarida la Forbes la nchini Marekani limemtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa Wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani. Huu ni msimu wa 18 katika muendelezo wa utoaji wa idadi hiyo na jarida la Forbes, ambapo Rais Samia ametinga ya idadi hiyo kwa mara ya kwanza.
Hii ni mara ya pili mfululizo jarida la Forbes limemtaja Rais Samia Suluhu Hassan katika namna mbili tofauti, mara ya kwanza ni kupitia Forbes Africa ambapo katika ukurasa wa 8 jarida hilo Rais Samia alipambwa kwa picha kubwa yenye kichwa cha habari kinachosomeka, “Aliuguza Taifa kwa huruma na ukakamavu zaidi”, hii ni katika kutambua mchango wake kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 nchini Tanzania pamoja jitihada zake kwenye kuimarisha uchumi.
Hivi leo tena tarehe 7 Desemba jarida hilo la Forbes, limemtaja tena Rais Samia Suluhu Hassan katika idadi ya wanawake 100 wenye nguvu zaidi dunia, huku 40 kati ya wanawake hao wakiwa wakurugenzi wa kampuni na taasisi kubwa duniani na 19 wakiwa ni marais wa nchi mbalimbali.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ni mara 3 pekee nafasi ya kwanza katika orodha hiyo haikushikwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ikiwemo mwaka huu ambapo nafasi hiyo imeshikwa na MacKenzie Scott, ambaye ni tajiri namba 3 Mwanamke duniani.
Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutajwa miongoni mwa Wanawake wenye nguvu zaidi duniani akitajwa katika nafasi ya 94 kati ya wanawake 100 walioorodheshwa. Forbes wameeleza kupitia tovuti yao kuwa, sababu kubwa ya Rais Samia kupata heshima hiyo ni kuwa, Rais Samia amekuwa nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 nchini Tanzania.
Wasifu wa Rais Samia Suluhu uliowekwa katika mtandao wa Forbes umeeleza kwa muhtasari na kumtambua Rais Samia kama Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa kwanza mwanamke Tanzania. Forbes wameongeza pia, mnamo mwezi Septemba mwaka 2021 Rais Samia amekuwa mwanamke wa tano kutoka barani Afrika kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo aliweza kuzungumzia usawa katika upatikanaji na ugawaji wa chanjo za UVIKO-19 duniani.
Hata hivyo, Forbes wamesema kuwa Rais Samia Suluhu amejipambanua na kujitofautisha na mtangulizi wake, ambapo amekuwa muumini mzuri wa sheria na taratibu zinazowekwa na Jumuiya za Kimataifa katika kupambana na UVIKO-19, ikiwemo kuruhusu chanjo, karantini kwa wageni waingiao Tanzania na uhimizaji wa matumizi ya barakoa.
Forbes wametoa angalizo kuwa, idadi hii haina uhusiano na nafasi ya mtu kisiasa wala hali yake ya kifedha, bali inatokana na jitihada na mchango mkubwa wa mfano mtu aliyoifanyia jamii yake.