Kuna hisia fulani nzuri hutujui siku ya Ijumaa, na kubwa hapa sio siku husika, bali ni wikiendi iliyo mbele yetu. Lakini kwa upande mwingine hali huwa tofauti siku ya Jumapili jioni, kuna hasira fulani, au kama sio
hasira kama ‘mood’ inapotea hivi kila kesho ni Jumatatu, siku ya kazi.
Kikubwa ni kwamba hakuna njia ambayo tunaweza kuimbia J’tatu, hapa wale waajiriwa wanaelewa zaidi J’tatu ni siku ya aina gani kazi. Ila sio mbaya, yapo mambo ambayo mtu anaweza kufanya siku moja ya J’pili na kuifanya J’tatu yake kuwa bora zaidi.
1. Andaa vipaumbele vyako vya J’tatu
Chukua dakika kadhaa siku ya J’pili, kaa chini na uandike vipaumbele vikubwa vitatu ambayo ungependa kuanza navyo siku ya J’tatu. Unaweza kufikiria kitu kama kujibu emails na meseji za wateja wako, au kumaliza viporo vya kazi ulivyoacha Ijumaa wiki ya jana. Kwa njia hiyo inaweza kukurahisishia kazi zaidi na kuifanya kuipenda J’tatu yako. Ni ngumu sana kuipenda siku ya J’tatu kama utafika kazi ukiwa hujui cha kufanya siku hiyo, hata kama kitakuwepo, lakini ni vyema kujua unaanza na kitu gani.
2.Pitia ratiba yako ya wiki nzima
Siku ya J’pili pitia ratiba yako ya wiki nzima, usifanye hiki kitu J’tatu asubuhi utaichukia kazi yako. Watu wengi hupenda kutazama ratiba zao za kazi siku ya J’tatu asubuhi, ikitokea amekutana na mlolongo wa vikao na mikutano mingi anaanza kuichukia hiyo siku na wiki nzima. Ni bora kupitia ratiba ya wiki nzima siku ya J’Pili kwani huandaa ubongo wako kisaikolojia kujua mambo unayokwenda kukutana nayo, hii ni silaha kubwa sana kwenye kuipenda J’tatu yako na wiki nzima kwa ujumla.
3. Panga na safisha unapoishi
Jumapili sio siku ya starehe pekee, sio siku ya kulala tu pia. J’Pili ni siku mahsusi kabisa ya kupanga unaianzaje J’tatu yako? Sasa basi, safisha chumba/nyumba yako. Panga nguo kabatini, fagia chumba, safisha choo na tandika kitanda chako kila wakati kinapochanguka. Haya mambo yanaonekana madogo kimtazamo, lakini yana mchango mkubwa sana kisaikolojia katika kuandaa bongo zetu kukabili mambo mbalimbali.
Ukiishi kwenye chumba safi, akili yako wiki nzima itanya kazi vizuri na kukuongezea nguvu ya kufanya mambo mengine kwa umakini zaidi. Hata ukiamka asubuhi siku ya J’tatu chumba chako kikiwa nadhifu, itakupa nguvu na hamasa ya kuianza J’tatu yako murua kabisa.
4. Panga nguo za kuvaa wiki nzima
Hebu angalia, kipi bora, kuamka J’tatu kuanza kutafuta nguo ya kuvaa, au kulala J’pili wakati unajua tayari kuwa kesho J’tatu nitavaa nguo kadha wa kadha? Uamkapo asubuhi siku ya J’tatu ubongo unakuwa na nguvu na mwepesi, usianze kuuchosha na mambo ya kuwaza nguo ya kuvaa, utaichukia siku nzima. Sio lazima sana kujua nguo za kuvaa wiki nzima, lakini angalau jua tu nitavaa nguo fulani, inakuwa rahisi kubadili mawazo pia huko mbeleni kama ulishapangilia.
5. Fanya Tahajudi (Meditate/Mediatation)
Sasa wakati umeshayafanya yote manne hapo juu, ni muda wa kutazama afya yako ya akili sasa, ni jambo la kuzingatia sana. Tajudi kama ni ngeni kwako, ingia Youtube andika (Meditation) utapata maelezo kwa kina. Lakini hii inasaidia sana kujenga afya ya akili.. hupunguza mkazo (stress), msongo wa mawazo, wasiwasi na hata woga usioelezeka.
Fungulia mziki laini, soma kitabu pendwa kwako au hata tembelea fukwe ya bahari au eneo lenye bustani safi na hewa safi, keti hapo na fanya tafakuri ya mambo mbalimbali na kuiweka sawa akili yako. Mazingira yanayotuzunguka yana nafasi kubwa sana katika afya ya akili zetu.