Watanzania watatu wamekamatwa nchini Uganda kwa shutuma za mauaji ya Emmanuel Deus mtunza fedha wa kampuni ya GEM James Gold Processing, Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda lilisema Deus alipigwa hadi kufa na kundi la raia la watanzania katika Halmashauri ya Mji wa Bukuya wilaya ya Kassanda.
Msemaji wa Polisi nchini Uganda Fred Enanga alisema kuwa Deus alikutana na kundi hilo la watanzania wanaojishughukisha na biashara ya dhahabu, wakinywa pombe huko Bukuya na waliingia katika ugomvi uliosababisha watuhumiwa hao kumpiga hadi kupoteza fahamu.
“Alikimbizwa katika kliniki ya Bukuya na baadaye marafiki zake walimhamishia katika hospitali ya rufaa ya Mityana. Alitangazwa amefariki dunia alipofikishwa katika hospitali hiyo kutokana na kuvuja damu nyingi eneo la kichwani” alisema Fred Enanga
Watuhumiwa watatu waliokamatwa kati ya hao sita ni Lubolo Erican, David Malingita na Peter Matunganjo. Pamoja na hayo Msemaji huo alisema vitendo hivyo vya vurugu, mashambulizi na kupigana vinawakumbusha hatari ambazo watu hukabiliana nazo wakati wa vurugu. Aliongezea pia kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutatoa ahueni kwa familaia ya marehemu huku washukiwa wengine wakiendelea kutafutwa.