Unaelewa nini ukisikia akiba ya fedha za kigeni, faida zake ni zipi kwenye uchumi?

HomeUncategorized

Unaelewa nini ukisikia akiba ya fedha za kigeni, faida zake ni zipi kwenye uchumi?

Rais Samia amehutubia taifa juzi katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka ambayo amegusia mambo kadhaa ikiwemo salamu za mwaka mpya, mafanikio ya serikali yake kwa kipindi cha miezi 9 iliyopita ya mwaka 2021 tangu aingie madarakani sambamba na kutaja baadhi ya mambo mengine yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2022, kwa mukhtasari ni hotuba iliyonesha mafanikio, matarajio na uelekeo.

Tukiwacha yote mengine, miongoni mwa mafanikio ya kiuchumi yaliyotajwa katika maelezo ya hotuba ni kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, jambo hili limeibua hamasa ya wengi kutaka kuelewa ni nini maana ya akiba ya fedha za kigeni ?, kwa mujibu wa hotuba ya Rais ya juzi akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kufikia kiasi cha dola bilioni 6.253 ( zaidi ya trilioni 14 tshs), kiasi hicho cha akiba kinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma mbalimbali kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha mieiz 7 ijayo. jambo hili linaingia katika rikodi, mara ya mwisho kwa akiba ya fedha za kigeni kufikia kiwango kama hicho ndani ya muda mfupi ilikua mwaka 2003.

Nimekusudia kueleza kwa lugha nyepesi kuhusu dhana nzima ya akiba ya fedha za kigeni ni nini maana yake katika ufafanuzi nilio ugawa katika nukta 7 muhimu kama ifuatavyo;

1. Nini maana ya akiba ya fedha za kigeni ?
Akiba ya fedha za kigeni ni kiasi cha jumla cha fedha za kigeni kinachoingia ndani ya nchi kupitia njia mbalimbali, mfano uuzaji wa bidhaa nje ya nchi (malipo katika pesa ya kigeni), shughuli za utalii (wageni wanapoingia wanakuja na pesa), uingiaji wa mitaji kutoka nje ( capital inflows eg, foreign direct investments), pia watanzania walio nje ya nchi wanaotuma pesa nyumbani (remittance, direct transfers), mfano nchi kama Pakistan ambayo ina diaspora kubwa nje ya nchi zaidi ya dola bilioni 1 inatumwa nyumbani kwa mwaka, n.k
Kwa ujumla akiba ya fedha za kigeni katika lugha ya kitaalamu ndio huitwa (foreign exchange reserves), akiba hiyo inatunzwa katika akaunti maalumu ya hifadhi ya fedha za kigeni ( foreign exchange reserve account) iliyopo benki kuu ya Tanzania BOT.

2. Fedha za kigeni ni zipi ? kwanini akiba ielezwe katika dola?.
Fedha za kigeni inaweza kuwa fedha ya taifa lolote, hivyo ukiwacha shilingi ya Tanzania ambayo ndio ina uhalali wa kutumika (legal tender) fedha nyengine zote zitakua za kigeni.
Lakini kwa muktadha huu akiba ya fedha za kigeni inakusudiwa kuwa ni fedha za mataifa ambayo ni washirika wakubwa wa kibiashara, au mataifa viranja katika uchumi wa dunia, au fedha zinazotumika kwa wingi katika mabadilishano ya biashara kimataifa kwa mfano dola USD, euro, dirham, yen, yuan n.k. kwa kuwa dola ya marekani ndio fedha inayotawala uchumi na biashara kimataifa (world reserve curency), akiba ya fedha za kigeni inawekwa katika dola, kwa mfano akiba yetu kwa sasa ni dola bilioni 6.253. ukiacha akiba hiyo viashiria vyengine vya kiuchumi vinavyoweza kuelezwa katika dola ni deni la taifa, pato la taifa GDP, bajeti ya serikali n.k.

Kufahamu zaidi kuhusu (dolar supremacy) na kutamalaki matumizi ya dola kimataifa rejea mkataba wa bretton woods agreement uliounda shirika la fedha IMF.

3. Akiba ya fedha za kigeni sio fedha iliyopo mfuko wa hazina ya serikali.
Jambo hili huwenda wengine wanalichanganya, lakini ilivyo ni kuwa akiba ya fedha za kigeni sio fedha iliyopo hazina. Kwa kawaida mapato yote ya serikali ya kodi ( kodi za mapato, kodi za majengo, tozo za miamala n.k) na yasiyo ya kodi ( faida za makampuni ya serikali, faida katika hisa za migodi, misaada, mikopo n,k) yanaingia moja kwa moja katika akaunti maalumu ya hazina ya serikali (exchequer account) inayosimamiwa na wizara ya fedha, hazina ndio ina jukumu la kugawanya fedha hizo (disbursement) kwenda katika matumizi mbalimbali kulingana na bajeti ya serikali inavyoelekeza, kwa mfano malipo ya mishahara, malipo ya wazabuni, mikopo ya wanafunzi, malipo ya deni la taifa, manunuzi ya silaha n.k. Wizara ya fedha ndio ina jukumu la usimamizi wa sera za kibajeti (fiscal policy), ambayo ni usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali kwa kutumia nyenzo mbalimbali.

Lakini akiba ya fedha za kigeni haipo hazina, akiba hiyo ipo katika akaunti maalumu (foreign exchange reserves account) iliyo chini ya benki kuu BOT, akiba ya fedha za kigeni inatumika katika mahitaji ya nchi kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, tutaeleza hili baadae.

Katika uendeshaji wa mfumo wa fedha ( monetary system) popote duniani wizara ya fedha inasimamia sera za kibajeti (fiscal policy) mapato, matumizi na muundo wake, benki kuu inasimamia sera za fedha (monetary policy), ugavi wa fedha katika uchumi, usimamizi wa mabenki, n.k, akiba ya fedha za kigeni ni moja ya nyenzo za sera ya fedha wanazotumia benki kuu katika usimamizi wa thamani ya fedha (exchange rate policy). tutaona baadae.

4. Akiba ya fedha za kigeni inatumikaje ? kuna umuhimu gani wa kuwa na akiba hiyo?
Kwa ujumla akiba ya fedha za kigeni inatumika katika kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, inaweza kutumika na serikali au na wananchi wa kawaida. Kwa mfano, mfanyabiashara anayetaka kuagiza mzigo wa nguo kutoka Dubai, au simu kutoka China atahitaji kubadilisha shilingi zake ili aweze kupata dola kufanikisha jambo hilo, atakwenda benki yeyote au maduka ya kubadilisha fedha (bureau de change), mabenki na maduka ya kubadilisha fedha yote yanapata fedha hizo kutoka benki kuu na na yanaratibiwa kwa kupewa leseni maalumu ya kufanya biashara hiyo, kwa serikali inaweza kutumia fedha za kigeni kuagiza vifaa mbalimbali, kulipia deni, kulipa (obligations) zozote za kimataifa. n,k.kukosekana kwa fedha za kigeni maana yake ni kukwama kwa biashara, uzalishaji na uchumi kwa ujumla.

Benki kuu ina uwezo wa kutambua kiasi cha fedha za kigeni kilichopo katika uchumi kupitia mtandao wa kibenki, maduka ya kubadilisha fedha, mifumo ya malipo electronic fund transfer n.k. na ndio maana inalazimishwa miamala kufanyika katika njia rasmi ili kuweza kurahisisha kukusanya takwimu.

5. Wakati gani akiba ya fedha za kigeni inaongezeka au kupungua ?, namna gani tunaweza kutafsiri hali hiyo?

a. Wakati akiba ya fedha za kigeni inapongezeka,
Kwa kuzingatia uwiano wa biashara (imports and exports), akiba ya fedha za kigeni zitaongezeka kwa wingi ikiwa nchi inauza zaidi kwenda nje ya nchi (exports), kwa mfano mauzo ya korosho, chai ,pamba, bidhaa za viwandani nk, yakiongezeka kwenda nje ya nchi fedha za kigeni zinaingia zaidi, hivyo kiasi cha malipo ya fedha za kigeni yanayofanyika kupitia njia mbalimbali za malipo kitaongezeka na takwimu za akiba ya fedha za kigeni itaongezeka.

Katika mfano mwengine, uuzaji wa huduma nje ya nchi kwa mfano shughuli za utalii ambazo kwa kiasi kikubwa inategemea wageni kutoka nje ya nchi, watalii wanapoongezeka kiasi cha fedha za kigeni ( wanachokuja nacho) kinachoingia nchini kinaongezeka, wapo wanaobeba cash au kuhamisha fedha hizo kwa njia za kibenki n.k.

Pia uwekezaji kutoka nje ya nchi (capital inflows), unapongezeka kiasi cha fedha za kigeni kinaongezeka kutokana na kuingia kwa mitaji hiyo ambayo ipo katika fedha za kigeni inaongeza akiba ya fedha za kigeni, n,k

b. Wakati akiba ya fedha za kigeni inapopungua;
Akiba ya fedha za kigeni inapungua katika matumizi mbalimbali ya kuagiza kutoka nje ya nchi, wafanyabiashara, serikali n.k, uagizaji wowote wa bidhaa kutoka nje ya nchi, mfano uagizaji wa nguo, petroli, vifaa vya ujenzi, kemikali za viwandani n.k serikali inapolipia malipo mbalimbali akiba inapungua, akiba inaweza kupungua pia ikiwa bidhaa inazouzwa nje nchi zimepungua bei sokoni malipo yanayopokelewa yatapungua hali kama hii huitwa (deteriorated terms of trade).

Nchi kuwa na hifadhi kubwa ya fedha za kigeni inategemeana na ukubwa wa uchumi na uzalishaji kwenda nje ya nchi ( productive capacity and diversified export structure), nchi inayozalisha na kuuza vitu mbalimbali inakua na vyanzo vingi vya uingiaji wa fedha za kigeni hivyo akiba inakua kubwa, kinyume chake ni kuwa nchi yenye uchumi mdogo wa uzalishaji uingiaji wa fedha za kigeni unakua mdogo na akiba yake ni ndogo. kwa ujumla mwenendo wa akiba ya fedha za kigeni inategemea na mwenendo wa biashara ya kimataifa wa nchi husika, mwenendo huo unaweza kueleweka kwa urahisi kwa kupitia takwimu za biashara ya kimataifa ( balance of payment statistics) ambazo huchapishwa na benki kuu ya Tanzania.

6. Akiba ya fedha za kigeni inatosha au haitoshi ?,namna gani akiba ya fedha inaweza kutafsiriwa inamudu matumizi ya nchi ?.
Kutosha kwa akiba ya fedha za kigeni inategemeana na mahitaji ya nchi kulingana na ukubwa ya uchumi wake, hivyo kujua kama hifadhi iliyopo inamudu mahitaji ya nchi inategemeana na vipimo (benchmarks) nchi ilivyojiwekea, kwa mfano, kwa mujibu kwa mwongozo wa utekelezaji wa sera za fedha katika wa ripoti iliyochapishwa na benki kuu BOT (monetary policy statement, june 2021/2022, uk 5), malengo ya sera ya fedha ni kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayotosha kuhudumia uagizaji wa bidhaa kwa kipindi cha miezi 4, akiba iliyopo hivi sasa kwa mujibu wa hotuba ya rais ya juzi inaweza kumudu uagizaji kwa kipindi cha miezi 7, hivyo kiasi kilichopo kinaweza kumudu mahitaji. Katika nchi za afrika mashariki na SADC kipimo cha miezi 4 mpaka 6 kinatumika kuonesha kama akiba ya fedha ya kigeni inamudu mahitaji ya nchi.

7. Akiba ya fedha za kigeni, inawezaje kutafsiriwa kiuchumi na kisera ?

a. Akiba ya fedha za kigeni ni ishara ya uchumi mkubwa,
Hifadhi ya kigeni inapokuwa kubwa ni ishara ya ukubwa wa muundo wa uchumi na nguvu za uzalishaji, nchi yenye hifadhi kubwa ya fedha za kigeni ni ishara ya kuwa na uzalishaji mkubwa mfano sekta kubwa ya viwanda, biashara, utalii, teknolojia inayopelekea mauzo kwenda ya nchi kuwa ni makubwa, Nchi ya China ina akiba ya fedha za kigeni dola trilioni 3.2 hadi kufikia mwezi novemba 2021, kwa mujibu wa tovuti ya takwimu mbalimbali za uchumi Trading economics, akiba hiyo ya Uchina ni mara 500 ukilinganisha na akiba ya Tanzania.

b. Akiba ya fedha za kigeni ni kiashiria cha ufanisi (indicator of perfomance),
Akiba ya fedha ya kigeni inaweza kuonesha ufanisi na mwenendo wa nchi kiuchumi na katika biashara ya kimataifa, kwa mfano katika kipindi cha miezi 9 iliyopita kuongezeka kwa akiba kumechangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji kutoka nje jumla dola bilioni 4 zimeingia kupitia miradi mbalimbali, kwa kuzingatia component inayonekana kuchangia ongezeko hilo tutasema uwekezaji kutoka nje unaongezeka, ikiwa uuzaji wa bidhaa za viwandani umeongezeka, mitaji imeongezeka na mengine, kwa ujumla akiba ya fedha za kigeni inaweza kutumika kuonesha ufanisi wa (sub sectors) za uchumi .

c. Akiba ya fedha za kigeni ni nyenzo katika kutekeleza sera ya udhibiti wa thamani ya fedha ( currency policy/ exchange rate policy).
Inapokuwa akiba ya fedha za kigeni ni kubwa uwezo wa nchi katika kusimamia udhibiti wa thamani ya fedha ya nchi dhidi ya nchi nyengine inakua kubwa, kwa mfano, inapotokea pressure ya kupungua thamani ya fedha ya nchi katika masoko ya fedha kimataifa ( currency depreciation) benki kuu inaweza kutumia akiba ya fedha ya kigeni kununua fedha yake kwa wingi sokoni ili ipandishe au ipunguze bei ya sarafu yake, nchi inaweza kufanya hivyo makusudi kununua na kuuza sarafu yake sokoni kwa kutumia akiba ya fedha za kigeni kwa malengo yeyote inayotaka, Nchi ya Uchina ni mashuhuri kwa hatua hizo, ( refer ; currency wars, currency intervention, currency manipulation etc).

d. Pamoja na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni lakini bado nchi inaweza kuwa na muundo mdogo wa kiuchumi na kukosa faida za uchumi ujumla.
Kwa mfano nchi inayozalisha na kuuza mazao ghali ya kilimo kwa wingi inaweza kupata fedha nyingi za kigeni na akiba kuwa kubwa lakini inakosa faida za ujumi jumla, kwa mfano kuuza mazao ghali maana yake imekosesha kuendelez viwanda vya ndani vya kuchakata mazao, imekosesha kodi ambazo zingepatikana katika mnyororo wa thamani, ajira ambazo zingepatikana kutokana na uanzishwaji wa viwanda n.k.

e. Nchi inaweza kuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni lakini bado muundo wa uzalishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi ni mdogo ( dependence/ non diversified).
Nchi inatakiwa kuwa na muundo wa uzalishaji wa vyanzo mbalimbali (diversified export structure) ili kuwa na ongezeko la hifadhi ya fedha za kigeni yeye uimara (resilient against shock), kwa mfano, nchi zinazouza kwa wingi mafuta zina akiba kubw aya fedha za kigeni lakini lakini kupungua kwa bei inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa, au nchi zinategemea utalii kama nchi za visiwa seychelles, mauritius , janga la corona ambalo limeathiri vibaya sekta ya utalii itapunguza kwa kiasi kikubwa uingiaji wa fedha za kigeni, hivyo inapendekezwa kuwa na diversified sector, kuliko kutegemea sana sekta moja.

error: Content is protected !!