Bei za mafuta zashuka

HomeKitaifa

Bei za mafuta zashuka

Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei za mafuta nchini.

Katika taaarifa yake iliyotolewa leo, mamlaka hiyo (EWURA) imeeleza kwamba,  ikilinganishwa na bei za mwezi Desema 2021, bei za Januari 2022 zitapungua kwa kati ya Shilingi 4 na 35 kwa lita ya petroli; na kati ya Shilingi 43 na 67 kwa lita ya dizeli isipokuwa kwa bandari ya Mtwara ambapo bei zitaongezeka kwa Shilingi 2 kwa lita; huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Shilingi 99 kwa lita.

Aidha, taarifa ya EWURA imefafanua kwamba bei za mafuta zingepungua zaidi iwapo thamani ya dola ya Marekani isingeongezeka dhidi ya Shilingi ya Tanzania ambapo dola ya Marekani imenunuliwa kwa Shilingi 2,314.23 ikiwa ni ongezeko la thamani kwa asilimia moja kutoka Shilingi 2,300.88 kwa dola.

Pia, EWURA wamesema kwamba kushuka kwa bei za mafuta kunachagizwa na maamuzi ya Serikali kupunguza tozo za taasisi za Serikali kwa lengo la kupunguza bei za mafuta hapa nchini. Kwa mujibu wa EWURA, maamuzi hayo yaliyofanyika mwezi Oktoba 2021, yamesaidia kupunguza bei za mafuta kwa kati ya Shilingi 23 na Shilingi 31 kwa lita kwa kutegemea aina ya mafuta na bandari yalipopokelewa mafuta hayo.

“Vilevile, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, Serikali iliahirisha ukusanyaji wa ada ya mafuta (petroleum fee) kuanzia Desemba 2021 na hivyo kufanya bei ya juu kufikiwa katika mwaka 2021 kuwa ni Shilingi 2,510 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam, Shilingi 2,525 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga na Shilingi 2,569 kwa lita ya petroli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara. Bila ya kufanya maamuzi haya, bei za mafuta zingefikia kiwango cha juu cha Shilingi 2,638 kwa lita ya petroli (Dar es Salaam), Shilingi 2,648 kwa lita ya petroli (Tanga); na Shilingi 2,693 kwa lita ya petroli (Mtwara).” wameeleza EWURA.

 

error: Content is protected !!