Hairat Muhina ni kati wa wanafunzi aliyefanikiwa kurudi Tanzania akitokea Ukraine alipokuwa akisoma mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Tiba Cha Kharkiv (KNMU), amewasili nchini juzi na kupokelewa na familia yake kwa machozi ya furaha, lakini hali yake ikabadilika ghafla.
Baba mzazi wa mwanafunzi huyo ambaye ni Kapteni Hanafi Muhina alisema hali ya mtoto wake ilibadilika walipofika nyumbani.
“Usiku (juzi) baada ya kutoka uwanja wa ndege , tulipofika hapa nyumbani alibadilika. Alikuwa analia sana, tukaona hali ile haikuwa ya kawaida , leo (jana) ameamka pia hayuko sawa na yuko chumbani muda wote hataki kuzungumza,”
“Tumebaini ile hali ya mapigano imemuathiri kisaikolojia, kwa sababu hajawahi kusikia wala kushuhudia mabomu na silaha zikipigwa. Nasema hivyo kwa sababu alipokuwa kule alishuhudia majengo ya nyumba za jirani yakilipuliwa kwa mabomu,” alisema Muhina, ambaye ni baba mzazi wa Hairat.
Aidha, baba wa Hairat amesema kwa sasa wanatafuta wataalamu wa saikolojia waweze kumsaidia binti yake huku akitoa rai kwa Serikali iendelee kuwasiliana na mamlaka husika ili kuwaokoa na kuwasaidia Watanzania wengine waliokwama warejee nchini.