BAKWATA yapoteza umiliki wa ekari 40

HomeKitaifa

BAKWATA yapoteza umiliki wa ekari 40

Mahakama Kuu Morogo Kitengo cha Ardhi imefulia mbali uamuzi wa Baraza la Ardhi na Makazi la Wilaya ya Kilombero uliotoa haki ya uamiliki wa ekari 40 za ardhi kwa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) katika kijiji cha Chita wilayani Kilombero Mkoani Morogoro.

Jaji Arafa Msafiri alifuta uamuzi huo baada ya watu wawili ambao ni Alfonzi Kakweche na Mgaigamba Kihakwi kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Baraza la Ardhi Kilombero kwamba kuna ukiukwaji wa sheria katika kutoa haki ya umiliki wa ardhi hiyo kwa BAKWATA na kwamba wao ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo.

Rufaa hiyo ilianisha makosa ya kisheria katika uamuzi wa Baraza la Ardhi na Makazi la Kilombero na Ulanga kwamba, baraza hilo halina uwezo wa kisheria wa kutoa maamuzi hayo. Jaji Arafa alisema kwamba Baraza la Ardhi lilifanya makosa kadhaa ya kisheria katika kutoa haki kwa BAKWATA kwenye umiliki wa ardhi hiyo.

> Wanakijiji wapiga mawe gari la Mkuu wa Wilaya

Jaji alisema kuwa rufaa iliyokatwa inasema kuwa BAKWATA ilinunua ardhi hiyo kwa shilingi 600,000/- ambapo manunuzi ya bei hiyo kisheria ni lazima yapitie kwenye Baraza la Kata ambalo kisheria, linapaswa kufanya maamuzi ya kuuza ardhi ya pesa isiyozidi shilingi milioni tatu. Kwa mujibu wa Jaji, hakukuwa na ripoti ya tathmini ya ardhi iliyofanywa ili kutoa thamani sahihi ya ardhi ambayo inatoa haki kwa Baraza la Wilaya kufanya maamuzi hayo.

Hivyo basi, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Morogoro, imetupilia mbali uamuzi wa Baraza la Ardhi Wilaya kwa kushindwa kujitosheleza kisheria katika kufanya maamuzi.  Shahidi wa upande wa mnunuzi (BAKWATA) alisadiki kwamba ardhi hiyo ilinunuliwa kwa shilingi 600,000 za kitanzania, kiwango cha fedha ambacho kiko nje ya mipaka ya kisheria inayotaka Baraza la Ardhi wilaya kuchukua hatua. Kiwango hicho cha fedha (600,000) kimo ndani ya mipaka ya Baraza la Ardhi la Kata na si la Wilaya.

Kulingana na Sheria ya Migogoro ya Ardhi ya Mwaka 2012, kifungu cha 33 (2) b, kinachosema kuwa Baraza la Ardhi na Makazi la Wilaya linapaswa kutoa uamuzi wa ardhi au mali isiyohamishika yenye thamani inayozidi shilingi milioni 50. Sheria hiyo kifungu cha 15 inasema kuwa ardhi ambayo thamani yake ni chini ya milioni 3, uamuzi wake utatolewa na Baraza la Kata, hivyo basi uamuzi wa Baraza la Ardhi la Wilaya kutoa uamuzi wa mali yenye thamani ya 600,000 imevunja sheria ya migogoro ya ardhi ya mwaka 2012 kifungu cha 15.

Kwa mantiki hiyo, sheria hiyo inavua uhalali wa BAKWATA kumiliki ardhi hiyo. Wakati wa kusikiliza shauri hilo, Kakweche amesema kuwa ardhi hiyo ni mali yake aliyoachiwa na wazazi wake ambao pia wamezikwa kwenye ardhi hiyo, na haikutelekezwa kama wanavyodai BAKWATA ambayo ilinunua ardhi hiyo 2007 kwa minajili ya kujenga shule.

Mahakama imetoa uamuzi kuwa rufaa hiyo ina mashiko na imefuta uamuzi wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kilombero.

error: Content is protected !!