Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amepokea rasmi nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Hungary nchini Tanzania, Mhe. Katalin Nyirati leo Februari 20, 2026.
Katika mazungumzo yaliyofuatia hafla hiyo, viongozi hao wameahidi kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na Hungary katika sekta za elimu, kilimo, maji na usafiri wa anga.
Tanzania na Hungary zinatarajia kusaini Hati ya Makubaliano kuhuisha Mpango wa Ufadhili wa Masomo kwa Watanzania kusoma elimu ya juu nchini Hungary kwa kipindi cha miaka mitatu 2027/29 ambapo idadi ya wanufaika wa ‘Stipendium Hunguricum Scholarship’ inatarajiwa kuongezeka kutoka 30 katika mpango wa sasa wa mwaka 2023/26.
Hivi karibuni, Tanzania na Hungary zitasaini Hati za Makubaliano katika sekta ya maji kukamilisha mradi wa Biharamulo. Ushirikiano huo utawezesha Tanzania kupata teknolojia za kisasa katika usafishaji na usambazaji maji kutoka Hungary. Vilevile katika sekta ya usafiri wa anga ili kuwezesha ushirikiano katika eneo hilo.
Aidha, katika sekta ya kilimo, Hungary itashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kubadilishana ujuzi na uzoefu ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi mkubwa na uwezo wa kujikita katika miradi mikubwa kitaifa na kimataifa.
Mhe. Kombo amempongeza Mhe. Nyirati kwa nafasi yake na kuahidi kuwa Tanzania itampa ushirikiano wa hali ya juu wakati akitekeleza majukumu yake nchini.



