Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema wilaya hiyo inatekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye jumla ya kilomita 146 kwa thamani ya Sh bilioni 140.
Amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan, na ujenzi huo unafanyika chini ya Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili.
Mpogolo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika ziara ya kukagua barabara zitakazonufaika na mradi huo. Alieleza kuwa kukamilika kwa barabara hizi kutapunguza adha ya wananchi kusafiri na pia kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa jiji.
“Katikati ya Jiji la Dar es Salaam tunajenga barabara zenye jumla ya kilomita 15. Tunamshukuru Rais Samia,” alisema Mpogolo.
Alitaja baadhi ya barabara zitakazojengwa kuwa ni Banana–Kitunda–Kivule hadi Msongola na Kivule–Majohe Njia Nne.
“Pia tutajenga Barabara ya Migombani–Kiwalani, Barabara ya Banana–Kitunda, na Barabara ya Baracuda–Chang’ombe hadi Majichumvi,” alieleza Mpogolo.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni Daraja la Majumba Sita–Segerea na Barabara ya Tabata–Maweni–Kisiwani.
Mpogolo aliwataka wakandarasi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati bila visingizio, ikiwemo visingizio vya mvua.
“Wakandarasi fanyeni kazi usiku na mchana. Dhamira ya Rais Dk. Samia ni kuona miradi hii inakamilika na iwanufaishe wananchi,” alisisitiza.
Mpogolo aliutaka uongozi wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Ilala kusimamia kikamilifu wakandarasi hao ili miradi ikamilike kwa viwango na kwa thamani ya fedha.
Mpogolo pia aliwaonya wananchi kuacha mara moja tabia ya kutiririsha maji machafu kwenye barabara, jambo linaloharibu miundombinu.
“Kuna watu wanapitisha maji yenye kinyesi kwenye mitaro ya mvua na barabara. Hii inaharibu barabara, mazingira na inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa,” aliainisha.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, Mhandisi John Magori, alisema mbali na barabara, pia wanajenga madaraja mbalimbali kupitia DMDP, ikiwemo Daraja la Segerea–Majumba Sita.
“Daraja hili lina urefu wa mita 80 na litagharimu Sh bilioni 7. Uko katika hatua ya kuweka nguzo ambapo litakuwa na jumla ya nguzo 54; kwa sasa tunaweka nguzo 27,” alisema Magori.




