P square jela maisha kwa kumbaka mtoto Coco Beach

HomeKitaifa

P square jela maisha kwa kumbaka mtoto Coco Beach

Mahakama ya Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemhukumu Dunia Suleman (36) maarufu kama P square, kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka nane.

Suleman, ambaye ni Beach Boy na mkazi wa Msasani wilaya ya Kinondoni, anadaiwa kumbaka binti huyo wakati akimfundisha kuogelea katika ufukwe wa Coco, uliopo Bahari ya Hindi.

Mshtakiwa huyo amehukumiwa kifungo hicho jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Erick Rwehumbiza, baada ya mshtakiwa huyo kukiri shtaka lake.

“Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka la kubaka mtoto, hivyo utatumikia kifungo cha maisha jela,ili iwe fundisho kwa wenzako” alisema Rwehumbiza.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali.

“Naomba mama wa mtoto huyu, anisamehe sana, nilipitiwa na shetani, naomba msamaha,” alidai mshtakiwa.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 13,2022 katika ufukwe wa Coco, uliopo wilaya ya Kinondoni baada ya familia mmoja kumpa watoto wawili akawafundishe kuogelea.

 

error: Content is protected !!