Wanafunzi 12,548 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hawatakosa sehemu ya kusomea baada ya halmashauri hiyo kukamilisha vyumba vya madarasa 110 vilivyokuwa vinahitajika kwa ajilia ya wanafunzi hao.
Jumla ya Sh2.2 bilioni fedha kutoka Serikali Kuu zimetumika kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo sanjari na samani zake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Mhandisi Modest Apolinary amesema walipokea kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 na ununuzi wa viti na meza 5,500 pamoja na ofisi tatu.
” Lengo ni kuwawezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023, kupata nafasi na kuanza masomo kwa wakati pamoja na kuwa na mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia,” amesema Alponary jana Desemba 23,2022 wakati wa kukabidhi vyumba hivyo.
Pamoja na kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo, halmashauri hiyo ilikuwa na uhitaji wa vyumba 252 kwa ajili ya wanafunzi hao na vilivyokuwepo ni vyumba 142 hivyo kufanya halmashauri hiyo kutokuwa na upungufu.
Mhandisi Apolinary amesema jamii pia ilishiriki katika mradi huo kwa kusaidia kutoa viashiria na nguvu kazi ambavyo vinakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya milioni 12, kama ishara ya kuunga juhudi ya Serikali.
“Tumeweza kutoa ajira fupi kwa wananchi 1,412, tumeweza kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, tumewezesha Serikali kupata kodi kutoka kwa mafundi na wazabuni waliouza vifaa vyao katika ujenzi huo,” amesema.
Pamoja na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo lakini wamekutana na changamoto ya kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, kukatika kwa umeme na upatikanaji wa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala, amesema kazi ya ujenzi wa vyumba hivyo wameifanya takriban siku 45 hadi 50.
“Wakati tunapewa fedha, tulipewa siku 75. Katika siku hizo wiki mbili Ilemela sisi tulikuwa bado hatujaanza kazi kwa sababu za kimfumo tulichelewa, lakini tulianza maandalizi mengine na tulipoanza kulikuwa hakuna kusimama mpaka leo hii tunapokamilisha hii kazi,” amesema Massala.
Amesema mbali na fedha hizo kutoka Serikali Kuu, pia kuna vyumba 126 vilijengwa na nguvu ya wananchi na wamevikamilishwa kupitia fefha za mapato ya ndani.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya amesema huo ulipatiwa Sh19.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 983.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, amesema kukamilika kwa madarasa hayo ni mafanikio ya miaka miwili ya Rais ambapo mwaka jana pia walipokea madarasa kama hayo yaliyotokana na fedha za Uviko-19.
“Katika Wilaya zote 7 za Mkoa wa Mwanza Ilemela mmewakanyaga wenzangu vibaya sana, wengine hata ukiwauliza nyie mnakabidhi lini madarasa lugha zinakuwa zinapiga chenga, hivyo Ilemela nawapongeza sana,” ameeleza Malima.