Msanii na mwanasiasa wa Upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ameutaka uongozi wa CHADEMA kuwekeza nguvu katika kukuza vijana huku akisema anaamini vijana ndio wanaojua kupambana kudai haki zao.
Akizungumza katika kikao cha baraza kuu la CHADEMA, Mlimani City jijini Dar es salaam kiongozi huyo amesema ipo haja ya vyama vya siasa hususani vya upinzani kuwekeza kwa vijana na kuwafundisha siasa za mageuzi.
“Pale ambapo tunapata changamoto, njia ya kutatua changamoto hizo ni kuwa wamoja na kukaa pamoja, hata wazee wetu walipokuwa wanapambana na ukoloni, pindi walipopata changamoto walikutana na kuungana na kisha kutatua changamoto hizo,” alisema Bobi Wine.
Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ambaye ni kiongozi wa chama cha National Unity Platform amesema ni wazo zuri kuwa na katiba mpya, lakini isichukuliwe kama ndio itamaliza matatizo yote kwenye nchi husika.
“Uganda tuna katiba nzuri sana, naweza kusema moja ya katiba bora zaidi duniani licha ya kuwa Jenerali [Rais Yoweri] Museveni amebadili katiba mara nyingi sana. Katiba yetu haiheshimiwi, sheria nchini Uganda ni nzuri tu kama ilivyo kwenye karatasi ilimoandikwa,” ameeleza.
Akitoa mbadala wa hayo amesema kuwa ni lazima kuwajengea uwezo wananchi waweze kuisimamia katiba ambayo wanakusudia kuwa nayo.