Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuwa tuzo za msimu wa 2020/21 zitakazotolewa na Shirikisho hilo zitatolewa Oktoba 21, 2021, kwenye ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dares Salaam.
TFF imeeleza kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa miguu nchini zitatolewa tuzo binafsi 56, ambazo ni tofauti na zile zinazotajwa kwenye kanuni kwa timu washindi wa Ligi mbalimbali. Taarifa ya Shirikiho hilo imefafanua kuwa kwa muda mrefu tuzo hizo zilikuwa zikihusisha Ligi Kuu pekee, lakini mwaka huu imebadili mfumo na sasa zitahusisha pia Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) pamoja na matukio mengine yan mpira wa miguu nchini na zitajulikana kama tuzo za TFF na zimewekewa vigezo maalum kwa washindi.
Pia imeelezwa kuwa kutakuwa na tuzo za kiutawala zikihusisha wasimamizi wa mpira wa miguu na wadau wengine wa mchezo huo hapa nchini, ambapo baadhi ya tuzo hizo ni tuzo ya Fair Play, Tuzo ya Rais wa TFF, Tuzo ya Mchezaji Gwiji, Tuzo ya Mhamasishaji Bora, Tuzo ya Kamishina Bora na Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja.
Tuzo ambazo zinatabiriwa kuwa na mvuto kutokana na ubora wa wanaowania tuzo hizo ni pamoja na tuzo ya Mchezaji Bora Ligi Kuu inayowaniwa na Clatous Chama (Simba), Mukoko Tonombe (Yanga) naJohn Bocco (Simba), tuzo ya Beki Bora Ligi Kuu inayowaniwa na Dickson Job (Yanga) na Shomari Kapombe na tuzo ya Kiungo Bora Ligi Kuu inayowaniwa na Clatous Chama (Simba) pamoja na Mukoko Tonombe na Feisal Salum (Yanga). Tuzo nyingine inayosubiriwa na wengi ni ile ya mchezaji Bora Ligi Kuu ya Wanawake inayowaniwa na Oppah Clement wa Simba Queens pamoja na Aisha Masaka na Amina Alli Bilali wote ya Yanga Princess.