Serikali kujenga chuo kikubwa cha TEHAMA nchini

HomeKitaifa

Serikali kujenga chuo kikubwa cha TEHAMA nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wiki ya Vijana na kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru zilizofanyika wilayani Chato mkoani Geita amesema Serikali inakusudia kujenga chuo kikubwa cha masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hapa nchini.

“Serikali inalenga kujenga chuo kikubwa cha Tehama. Tutatoa kipaumbele kwenye masuala ya utafiti na ubunifu kwenye Tehama. Chuo ambacho nadhani kwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Tanzania itakuwa inaongoza,” amesema Rais Samia.

> Ahadi 6 za Rais Samia kwa wakazi wa Chato

Kwa kutambua umuhimu wa TEHAMA, Rais Samia amesema Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye simu janja, vishikwambi na modemu ili kuwajengea vijana mazingira ya kujiajiri kwa maendeleo yao.

Pia Rais Samia amewaasa vijana kuzingatia matumizi sahihi ya TEHAMA ili kupusha migongano na machafuko.

“Licha ya faida ya TEHAMA, ikitumika vibaya inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo mifarakano, vurugu, machafuko, vita na pia kuongezeka vitendo viovu kama vile wizi, ugaidi, utakatishaji fedha na kadhalika.” alisisitiza Rais Samia

error: Content is protected !!