Wizara ya Afya nchini Tanzania imewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Uviko-19 ikiwemo kupata chanjo kwa sababu ugonjwa huo bado upo.
Kati ya Mei 5 hadi Juni 3, Wizara hiyo imeripoti jumla ya visa vipya 160 ingawa hakujaripotiwa kifo chochote katika miezi miwili iliyopita.
Taarifa hiyo ya wizara hiyo iliyotolewa Juni 7, 2022 imeainisha mikoa ambayo imeripoti kiwango kikubwa cha maambukizi ambapo Dar es salaam imeripoti visa 130, Arusha (10), Mwanza (5), Shinyanga (4), Mtwara (3), Dodoma (2) na Mara ni visa viwili.
Waliopata chanjo kati ya Mei 5 mpaka Juni 3 ni 775,680 huku wagonjwa watatu waliothibitika kuwa na maabukizi na kulazwa wote walikuwa hawajapata chanjo hivyo wizara imeendelea kusisitiza wananchi kupata chanjo kamili ya Uviko-19.
Kujikinga na ugonjwa huo, wananchi wametakiwa kupata chanjo, kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.