Mradi wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite mkoani Dar es Salaam unaosimamiwa na serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), umefikia asilimia 93, na Desemba mwaka huu litaanza kutumika.
Akizungumza baada ya kuweka zege la mwisho katika ujenzi wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema mradi upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Ameeleza kuwa, Desemba mwaka huu, wanatarajia kuukamilisha na magari kuanza kupita pamoja na watembea kwa miguu. Akifafanua baadhi ya faida za mradi huo, Mhandisi Mativila amesema changamoto ya msongamano wa magari inayolikabili daraja la awali katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, itakuwa historia.
“Ule msongamano mkubwa uliokuwa ukilikabili daraja dogo la zamani la Selander hautakuwepo tena, kwa sababu daraja hili jipya litatumika pamoja na la zamani,” amesema.