Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kati ya Desemba hadi Januari mwaka 2023, daraja la juu makutano ya barabara za Kilwa na Mandela eneo la Uhasibu itaanza kupitisha magari pande zote mbili.
Kwa sasa daraja hilo na lile la Veta- Chang’ombe yanapitisha magari upande mmoja, hatua inayotajwa kupunguza foleni kwa watumiaji barabara za Nyerere, Mandela na Kilwa.
Profesa Mbarawa alieleza hayo jana, wakati akikagua ujenzi wa barabara za mwendokasi awamu ya pili. Pia alikagua ujenzi wa daraja eneo la Gerezani, Veta- Chang’ombe.
Kwa upande wa Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Barakael Mmari alifafanua kuhusu mwonekano wa daraja hilo kuwa limesanifiwa kwa sababu maalumu, likiwa na njia mbili na limejengwa katika maeneo mawili tofauti na upande wa katikati itajengwa barabara ya mwendokasi.