Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Verronica Kessy amewaonya akina mama (wanawake watu wazima) wanaojihusisha kimapenzi na wavulana wadogo (vibenteni) akisema huo ni ukatili wa kingono dhidi ya watoto unaoangukia kwenye makosa ya ubakaji.
“Ukatili huu wa kingono hujumuisha vitendo ambavyo havihusishi sana vitendo vya kushurutisha au vitisho, bali ni vile ambavyo vinaweza kufanywa kwa njia ya maneno ya kubembeleza, hongo, utii, hadhi, mamlaka, na kupotosha desturi za kijamii,” alisema.
Akikemea matukio hayo kwenye maadhamisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika Kata ya Migoli wilayani Iringa, Kessy alisema katika mazingira hayo mhusika (mtoto) anaweza asitambue ukatili huo wa kingono unaofanywa dhidi yake.
“Kama nchi tunapaswa kuchukua hatua dhidi ya ukatili huu ambao pia uwaathiri sana watoto wa kike na kujumuisha kujamiiana kwa ndugu wenye uhusiano wa damu, ubakaji na ulawiti,” alisema huku akiwataka wadau kutoa taarifa za matukio ya aina hiyo ili mamlaka ziweze kuchukua hatua za kisheria.
Mkuu wa Wilaya amewasihi wazazi na walezi kuwa makini katika kusimamia malezi ya watoto wao kwa kujua michezo wanayocheza na aina ya marafiki wanaoambatana nao kwani jamii ya sasa imechafuka kimaadili.
“Wazazi na walezi tengeni muda wa kuzungumza na watoto wenu na msikubali watoto wenu walale na watu msiowaamini ili kuisaidia nchi kukabiliana na kukomesha ukatili wa kingono,” alisema.
SOURCE: Habari Leo