Elon Musk kuuza hisa za Tesla kutatua tatizo la njaa duniani

HomeKimataifa

Elon Musk kuuza hisa za Tesla kutatua tatizo la njaa duniani

Elon Musk, tajiri namba moja duniani amewapa mtihani Shirika la Chakula Duniani (WFP) kuthibitisha kwamba $6 Bilioni za kimarekani zinaweza kutatua tatizo la njaa duniani. Elon aliyasema hayo wakati akijibu ujumbe wa David Beasley, Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani, uliosema kuwa matajiri wakubwa kama Elon Musk wawe mstari wa mbele katika kutatua matatizo ya dunia kama njaa.

Beasley alisema kuwa “Kiasi cha shilingi trilion 13 tu zinatosha kabisa kuokoa maisha ya watu milioni 42 duniani wanaotaabika na baa la njaa”… Elon alijibu ujumbe huo na kusema kwamba, “Kama WFP wataweza kuthibisha kupitia kwenye huu ukurasa wangu wa twitter ni namna gani wataweza kuondoa njaa duniani kwa $6 bilioni basi nitauza hisa za Tesla mara moja na kutoa fedha hiyo”.

Elon Musk ni Mkurugenzi wa kampuni ya magari yatumiayo umeme (Tesla) ambapo wiki iliyopita kampuni hiyo iliungana na kampuni nyingine duniani kwenye orodha ya kampuni yenye thamani $1 Trilioni.

Kwa mujibu wa jarida la Bloomberg, Elon Musk utajiri wake ni $311 bilioni, kutoa $6 bilioni ni kiasi kidogo sana cha fedha kwake, kwani Oktoba 29 mwaka huu pekee, utajiri wake uliripotiwa kupanda kwa $9.3 bilioni kwa mujibu wa ‘Bloomberg Wealth Index’.

error: Content is protected !!