Epuka matumizi ya mate wakati wa kujamiiana

HomeElimu

Epuka matumizi ya mate wakati wa kujamiiana

Wakati matumizi ya mate yakiwa maarufu kwa wengi wakati wa kujamiiana, hasa yanapotumika kama aina fulani ya kilainishi hasa ukeni na hivyo kuleta ladha ya tendo, habari si njema sana kwa watumiaji wa mate hayo wanapoburudika.

Wataalamu wa afya wamesema kuna ongezeko la magonjwa yanayosababishwa na maambukizi ya fangasi na bakteria katia njia ya uzazi vya mwanamke, huku chanzo kikubwa kikitajwa kuwa ni mate.

Sayansi inaeleza kuwa kinywa cha binadamu kimeundwa na mamia ya backeria ‘oral microflora’ ambao ni rafiki kwa afya ya kinywa, hata hivyo wana madhara iwapo wataenda ukeni.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake katika hospitali ya Salaaman iliyopo Temeke, Abdul Mkeyenge alieleza kuwa kuna bakteria ambao makazi yao ni huko, hivyo wanaotumia mate kama kilainishi wanakosea.

“Kisayansi mate hatuyatumii kama kilainishi katika kufanya tendo la ndoa kwa kuwa kwenye kinywa kuna bakteria tofauti, hivyo unapotumia mate kama kilainishi kuna faida za wakati huohuo, lakini utakuwa unawahamisha wale bakteria kuja ukeni,kwa hiyo madhara yake ni maambukizi,” alisema Dk. Mkeyenge.

Alisema wapo wanawake wanaopata madhara makubwa zaidi, ikiwamo kutokwa na maji machafu wakati wa tendo na hivyo kupoteza thamani yao na kuonya kwamba wasipopata matibabu kwa wakati tatizo huwa kubwa zaidi.

Nini kifanyike?

Dk Mkeyenge alisema wanaume wanatakiwa kuwaandaa wenza wao wakati wa kufanya tendo la ndoa.

“Wengi wanapokuwa na wenza hawaandaani vizuri, baadaye wakati wa tendo unakuta anakuwa mkavu hajapata ute ambao ndiyo kilainishi kutoka mwilini.

“Ukimwandaa vizuri kuna majimaji ambayo anaweza kuyatoa ndiyo yanayosaidia kulainisha sehemu za siri hata baadaye ukija kumwingilia hatahisi maamivu yoyote wala karaha,” alisema Dk Mkeyenge.

Sababu 5 kukosa ute

  1. Kukosa hisia na hamu ya tendo 
  2. Kuhisi maumivu wakati wa tendo
  3. Uwepo wa damu baada ya tendo
  4. Hedhi kukosa mpangilio maalum
  5. Matumizi ya uzazi wa mpango na vidonge vya P2, vitanzi, sindano.

 

error: Content is protected !!