Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuwaongoza Watanzania kupokea ndege ya kwanza ya mizigo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 767-300F leo Juni 3, 2023 katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Ndege hiyo ya mizigo ambayo ni ya kwanza kununuliwa Tanzania inatarajiwa itakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara waliokuwa wanakumbana na changamoto za usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi na kulazimika kutumia nchi jirani ambako gharama huwa juu.
Ununuzi wa ndege hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha utendaji kazi wa ATCL ambapo kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa, tayari malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa ndege mbili za Boeing 737-9, ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400, na ndege moja Boeing 787-8 yameshafanyika.
Ni mtoto wa matoleo ya Boeing 767.
Kampuni ya ndege ya Boeing ya Marekani ilianza kuzalisha matoleo ya Boeing 767 mwaka 1993 baada ya kupokea oda ya ndege 60 za mizigo kutoka kwa Serikali ya Marekani, ambapo iliingia sokoni rasmi mwaka 1995 baada ya kukamilika kwa majaribio yake.
Modeli zilizopita za muundo huo ni pamoja na 757-300 , 757-200, pamoja na 747 ambazo zimekuwa zikifanyiwa maboresho kwa nyakati tofauti ili kuendana na mahitaji ya soko.
Ndege hiyo imeboreshwa kutoka kwenye ndege za abiria za modeli ya 767 ambayo ni kuongezwa ukubwa wa tenki la mafuta, uwezo wa kukaa angani pamoja na kutengenezwa kwa madini ya alminiamu yaliyoifanya ndege hiyo kuwa nyepesi kuliko nyingine za kundi hilo.
Sifa za jumla
Kwa mujibu wa Boeing ndege ya 767-300F ina uwezo wa kubeba tani 54 za mizigo na kukaa angani kwa muda wa masaa 10 bila kutua jambo ambalo litaifaidisha Tanzania ambayo huzalisha tani 24,941 za maua, mbogamboga, nyama na samaki kwa mwaka ambapo ni tani 420 pekee zilisafirishwa kutokea nchini.
Spidi ya uhakika
Ukiachana na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa ndege hiyo kasi yake si ya kutilia shaka kwani ina uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 850 kwa saa moja.
Umbali ambao ndege hiyo inaweza kwenda kwa saa moja ni sawa na ule wa kutoka Dar es Salaam mpaka Mbeya ambapo magari ya kawaida hutumia kati ya saa 10 hadi 12.
Rafiki wa mazingira na uchumi
Pamoja na kwamba tenki lake la mafuta linabeba lita 90,770 Boeing wanabainisha kuwa kasi yake ya utumiaji wa mafuta ni wa chini kwa asilimia nne kulinganisha na ndege nyingine za aina yakekutokana na maboresho yaliyofanywa kwenye injini.
Maboresho yaliyofanywa yanatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 20 tofauti na ndege nyingine kama 707 na DC-8. Pia ndege hiyo ni rafiki wa mazingira kwani haitoi kiwango kikubwa cha kelele.
Mkombozi wa wakulima na wafanyabiashara
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Juni Mosi, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema ujio wa ndege hiyo utawanufaisha wakulima na wafanyabiashara nchini.
“Ujio wa ndege hiyo kutaleta manufaa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya mbogamboga, maua, nyama samaki, madini na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na serikali pamoja na wafanyakazi hususani madawa ya hospitali”, amesema Prof Mbarawa
Mbarawa ameongeza kuwa wanatajaria kutumia ndege hiyo kuhudumia usafirishaji katika vituo vya kikanda na kimataifa kama vile Nairobi, Dubai, Guangzhou, Harare, Kinshasa pamoja na Mumbai.
SOURCE : NUKTA HABARI