Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema mageuzi ya kimfumo pamoja na usimamizi thabiti wa sheria ndio vitu vitakavyosaidia kupambana na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu na kuisababishia Serikali hasara.
Rais Samia aliyekua akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/22 leo March 29 2023, Ikulu jijini Dar es Salaam amewaambia Watanzania ili rasilimali za nchi zitumike inavyopaswa inatakiwa kutumia mifumo imara na kuwa na nidhamu.
“Ni kutumia mifumo na kuwa na nidhamu, ili tuweze kuondoa hali iliyopo, hatusimamii nidhamu kwa sababu sisi wenyewe ni wanufaika, niwaombe sana nchi hii tukisimamia vizuri rasilimali huko mbele tutapunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za mikopo.
“Tutakopa pale itakapokuwa lazima pekee, twendeni tukasimamie rasilimali, ukusanyaji na matumizi yake, “ amesema Rais Samia.
Rais Samia aliyeonekana kukasirishwa na baadhi ya mambo yaliyoibuliwa katika ripoti ya CAG, pamoja na mambo mengine ametaka kufanyika mabadiliko katika mambo yafuatayo.
Mifumo ya ukusanyaji mapato bandarini
Kwa mujibu wa Rais Samia, mapato ya bandari ya Dar es Salaam yanaweza kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya bajeti ya taifa ikiwa tu kutakuwa na usimamizi imara wa ukusanywaji wa mapato.
Kutokana na hilo ameziagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha wanaoanisha mifumo yao, ili kurahisisha shughuli ya ukusanyaji na ufuatiliaji wa mapato.
“Nawataka TRA na TPA kuhakikisha mifumo inasomana. Nimeambiwa TRA kuwa Wakorea wamekuja kwa ajili ya mifumo wasiondoke mpaka kuhakikisha hili linaisha,” amesema Rais.
Aidha, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema tatizo la mifumo bandarini linaweza kutatuliwa kwa kuikaribisha sekta binafsi kufanya uwekezaji katika teknolojia pamoja na usimamizi wa mifumo.
Upotevu wa fedha katika halmashauri
Kutokana na zaidi ya halmashauri 14 kupata hati zenye shaka huku halmashauri ya Ushetu ikipata hati mbaya, Rais Samia amemtaka Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Anjellah Kairuki kuharakisha urasimishaji wa mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri.
Mfumo huo mpya unaoitwa Tausi unatajwa utasaidia kupunguza ubadhirifu wa fedha za kodi zinazokusanywa ambazo wakati mwingine huibiwa kabla hazijawasilishwa Serikali Kuu.
Pamoja na kuboreshwa kwa mifumo ya ukusanyaji, Rais Samia ameagiza wale wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za halmashauri zikiwemo za mradi wa Uviko-19 kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Mashirika ya umma kutupiwa macho
Ripoti ya CAG imebaini mashirika ya umma yameendelea kupata hasara mfululizo badala ya faida jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji kwa Serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22 shirika la ndege ATCL lilipata hasara ya Sh 35.1 ambapo kwa mwaka 2020/21 lilipata hasara ya Sh 36.2 huku Shirika la Reli TRC likipata hasara ya Sh 31.29 bilioni kwa mwaka 2021/22.
Kutokana na hayo Rais Samia ameagiza kufanyika kwa tathmini ya kina juu ya manufaa ya mashirika ya umma ambayo yanapaswa kubaki au kuondolewa kwa sababu yamekuwa yakitengewa bajeti za uendeshaji kila mwaka lakini hayarudishi faida serikalini.
Ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi
Kupitia ripoti ya CAG imebainika kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa makusudi wa malipo kwa wakandarasi waliomaliza majukumu yao jambo ambalo na kusababisha riba na kuiongezea gharama Serikali.
Mathalan, ripoti ya CAG imeeleza kuwa Sh414 bilioni zililipwa kama riba kutokana na kucheleweshwa kwa malipo kwa wakandarasi waliomaliza majukumu yao kwa wakati.
Rais Samia amewaagiza makatibu wakuu wa wizara mbalimbali kuhakikisha hilo linatokomezwa kwani siyo tu linaongeza gharama za Serikali bali pia linaua wawekezaji wa ndani ambao wanategemea fedha za malipo ili waweze kukua.
Usimamizi wa sheria
Kukosekana kwa usimamizi thabiti wa sheria kwa wale wanaobainika kufanya ubadhirifu kunatajwa kama sababu ya matukio hayo kuendelea kujitokeza katika ripoti za CAG kila uchwao.
Rais Samia amezikumbusha mamlaka za sheria ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kulivalia njuga suala hilo ili fedha za umma zisiendelee kupotea.
Pamoja na kupokea ripoti ya CAG Rais Samia amepokea pia ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) ambapo ameishukuru taasisi hiyo kwa kufanya wajibu wake wa kuzuia vitendo vya rushwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amesema katika kipindi cha mwaka 2021/22 Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh14.2 bilioni na Dola 14,571 za Marekani kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi.
Sh8.4 bilioni ya fedha hizo zilitokana na ukwepaji kodi ambapo ziliingizwa katika akaunti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).