Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) imezindua rasmi Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZs) yenye lengo la kuvutia wawekezaji wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara barani Afrika.
Akizungumza jana Agosti 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema maeneo hayo yameunganishwa na miradi mikubwa ya miundombinu kama reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), barabara, bandari na viwanja vya ndege ili kuwezesha shughuli za kibiashara.
Ametaja maeneo ya kimkakati kuwa ni Nala SEZ (Hekta 607), Kwala SEZ (Hekta 40.5), Buzwagi SEZ (Hekta 1,333), Bagamoyo Eco Maritime City SEZ (Hekta 151) na upanuzi wa Benjamin William Mkapa SEZ.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Tausi Kida amesema kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji inalenga kuongeza ajira, mauzo ya nje na kuimarisha uhamisho wa teknolojia kutoka kwa wawekezaji kwenda kwa Watanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Giread Teri amesema serikali inatoa maeneo hayo bure kwa wawekezaji wa viwanda ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza mauzo ya nje.
“Tunataka Tanzania isiwe soko tu la bidhaa za viwandani kutoka nje, bali iwe mzalishaji mkubwa,” amesema.