Urembo siyo hali ya kuwa na mvuto pekee bali urembo unajumuisha pamoja na kuendana na vitu vyote unavyovaa. Inapaswa nguo ikae mahala pake, nywele ziwe mahala pake vivyo hivyo kunukia vizuri, tabasamu, na hata namna ya kutembea. Wanasaikolojia wanaeleza kuwa unaweza kubashiri umaridadi wa mtu kwa kuangalia viatu vyake.
Ili kutokufanya kiatu chako kikuharibie muonekano wako, hizi ni baadhi ya dondoo unazopaswa kuziangazia.
1. Vaa viatu vinavyokutosha
Kila siku unatumia miguu yako kutembea hivyo uzito wa mwili wako wote, unaishia kwenye miguu hiyo. Kuvaa viatu ambavyo havikutoshi ama haiikukai vizuri vinaweza kukupa tafrani ya namna fulani ikiwemo miguu kuuma na hata kuchubuka kutokana na kubanwa na pengine kuharibu kabisa namna unavyotembea
Tovuti ya Fairview imeandika “Usinunue viatu kutokana na saizi peke yake. Inashauriwa kujaribu viatu kabla ya kununua kwani saizi hutofautiana kulingana na kampuni inayotengeneza viatu.”
2. Vaa kiatu kutokana na sehemu unayoenda
Kuna viatu kwa ajili ya kila sehemu, hapo wabunifu hakika wametufaa. Vipo viatu vya ufukweni, viatu kwa ajili ya kutoka ‘out’ na hata viatu kwa ajili ya kwenda kuwasalimu wakwe. Kila mtu ana uwanda mpana sana wa kuchagua na utaonekana mtu wa ajabu utapakovaa viatu vya mchuchumio ‘high heels’ na kwenda navyo ufukweni.
3. Vaa viatu kulingana ana afya yako
Afya ina mawanda mapana sana. Kuanzia afya ya mwili na mambo mengine ikiwemo akili na ngozi. Baadhi ya watu afya yao ya miguu ina changamoto na hivyo miguu yao hutoa harufu mbaya, hivyo kiatu sahihi kinaweza kuwa msaada kwa watu wenye changamoto mbalimbali ikiwemo kiharusi na magonjwa mengine.
Pamoja na hayo yote, unapovaa kiatu, zingatia kama vinaendana na mavazi yako. Mfano, viatu vya ofisi hupendeza zaidi vinapovaliwa na mavazi ya kiofisi huku kwa mavazi ya kawaida (casual) yakiwa na machaguo mengi kwa ajili ya kuendana nayo.