Fanya mambo haya kila Jumatatu asubuhi ili uwe na mafanikio

HomeElimu

Fanya mambo haya kila Jumatatu asubuhi ili uwe na mafanikio

Usingizi wa Jumatatu asubuhi unaweza kukupa ugumu sana kukiacha kitanda chako na kwenda kwenye majukumu yako. Ndio maana sio ajabu kusikia watu wengi wakisema hawaipendi siku ya Jumatatu.

Hata hivyo huwezi kuiepuka Jumatatu, badala ya kuichukia ni vyema ukawa na mipango imara ili siku hiyo iwe mwanzo wa wiki njema. Jumatatu lazima iwe mwanzo wa mafanikio yako katika kila wiki.

Click Habari inakushauri kuhakikisha unafanya mambo yafuatayo kila asubuhi ya Jumatatu, ili uwe na wiki yenye mafanikio;

1. Amka mapema

Watu wengi hupata ugumu kuamka mapema siku ya Jumatatu. Wengine huwa na sababu kama kuchelewa kulala Jumapili kutokana shughuli mbalimbali za kijamii.

Hata hivyo, iwapo utafanikiwa kuamka mapema, utajisikia fahari na utayari kwamba wiki hiyo mambo yako yataenda kwa wakati.

Iwapo unaamini ukichelewa kulala utashindwa kuwahi kuamka, hakikisha unalala mapema siku ya Jumapili na usiache kuweka kengele (alarm) kwenye kifaa chako (simu au saa).

2. Mazoezi 

Huhitaji kwenda ‘gym’ au kukimbia umbali mrefu kama Wanariadha wa mashindano ya ‘Olympic’. Unaweza kufanya mazoezi mepesi ya kunyoosha viungo vyako ukiwa hata chumbani.

Mambo yamerahishwa siku hizi, unaweza kupata maelekezo ya namna bora ya kufanya mazoezi mepesi kupitia mtandao. Ingia ‘Youtube’ na kwenye mitandao mingine kufanikisha hili.

Mazoezi yatailinda afya yako, lakini pia yatakupa ari kwenda kupambana.

>Usithubutu kufanya mambo haya 5 ‘wikiendi’ hii

3. Vaa vizuri

Mavazi yana nafasi katika kuongeza kujiamini, na Jumatatu asubuhi ni wakati ambao unahitaji kujiamini kwako kuwa katika ubora wake.

Hata kama unavaa mavazi ya kazi, vaa mavazi masafi uwe nadhifu. Kama unakwenda ofisini ‘tungua’ zile nguo za kupendeza zaidi uvae upendeze.

Katika hili, ni muhimu sana kuandaa mavazi yako Jumapili ili Jumatatu usipoteze muda kuanza kutafuta nguo za kuvaa

4. Hakikisha umeacha nyumba au chumba chako katika hali ya usafi

Usiondoke bila kutandika kitanda chako. Hakikisha maeneo yote ya ndani kwako ni masafi ndipo uondoke.

Jambo hili ambalo linaongeza pia umuhimu wa kuwahi kuamka, litakuongezea kujiamini na furaha moyoni.

5. Salimia watu

Usianze wiki bila kufahamu hali za wafanyakazi wenzako, washirika wako katika kazi, viongozi wako na wengine wanaohusika kwenye kazi yako.

Hakikisha umewajulia hali baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki.

6. Panga vizuri ratiba yako huku ukiwa tayari kwa mambo ya dharura.

Ni vyema ukapanga mambo yako, fahamu unayotaka kufanya kwa wiki nzima.

Hii itakusaidia kufahamu mambo ambayo hujakamilisha na kuwa na mkakati mzuri wa utekelezaji.

Hata hivyo, kuna mambo ambayo yanaweza kutokea bila wewe kupanga. Ni vyema katika kupanga ratiba yako, ukawa na utayari kwa ajili ya kushughulika na mambo ya dharura yanapojitokeza.

7. Kumbuka kwamba kuna Jumanne

Huwezi kumaliza mambo yote Jumatatu. Jipange kwa kiasi, jipe muda wa kumaliza mambo uliyokusudia, yale yasiyowezekana yatafanyika siku inayofuata

Pia, usiache kusali kwa imani yako ili Mungu akuongoze katika kazi zako.

error: Content is protected !!