Huduma za kibingwa za Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), zitaanza kutolewa katika hospitali mpya ya kisasa ya Rufaa Kanda Mtwara, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Abbas Ahmed, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara, ambayo itahudumia wakazi wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na mataifa jirani.
“Hospitali hii haitahudumia wakazi wa mikoa ya kusini peke yake, tunatarajia wagonjwa kutoka Msumbiji, Comoro na hata Malawi, hivyo ujio wa huduma za MOI utachagiza utalii wa matibabu hapa na kubwa zaidi ni huduma zimesogezwa karibu na wananchi, pasipo kulazimika kufuata huduma hizo Dar es Salaam,” alisema Kanali Ahmed.
Amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo, ambapo mtambo wa kisasa wa CT-Scan umeshawasili kwa ajili ya usimikaji, mashine ya X-ray imeshasimikwa na mashine ya kisasa ya MRI itawasili hivi karibuni.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara , Abdallah Malela, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface, kwa muitikio wake wa kufika Mtwara, ili kuona namna bora ya kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara katika kuanzisha huduma za kibingwa za Mifupa.
Naye Dk Respicious Boniface, amasema MOI inatekeleza kwa vitendo agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zinazogezwa karibu na wananchi, ambapo katika mikoa ya kusini tayari huduma za MOI zinapatikana Hospitali za Nyangao Lindi pamoja na Ndanda.