Huku wengi wakitafuta usafiri kununua ili kurahisisha mizunguko ya hapa na pale, wengi huwaza kwanza magari ya kifahari ambavyo pia gharama zake zipo juu na baiskeli kuonekana kama usafiri wa wale wasio na uwezo wa kununua magari hayo ya kifahari.
Umeshawahi kujiuliza endapo kuna baiskeli za hadhi unayoitaka ama kuwa uendeshaji wa baiskeli unaweza kukusaidia kuepuka foleni huku ukikusaidia pia kufanya mazoezi na kuimarisha afya yako?
Unaweza kushangaa ila “Beverly Hills Edition” ama “fat bike” kwa sasa ndiyo baiskeli ghali zaidi duniani. Baiskeli hiyo imetengenezwa kwa dhahabu ya kareti ishirini na nne (24k) na ina thamani ya dola za kimarekani milioni moja ($ 1M) sawa na shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania (2,318,000,000).
Baiskeli hiyo imetengenezwa na kampuni ya Hugh Power kwaajili ya waendesha baiskeli milimani ama huitwa ‘mountain bike’ imeunganishwa na teknolojia ya hali ya juu ambapo kila kipande cha baiskeli hiyo kimethibitishwa ‘certified’, kuwekwa nembo maalum, urembo wa almasi pamoja na viti vilivyotengenezwa na ngozi ya mamba.
Gharama ya baiskeli hii moja inaweza kununua V8 takribani 11 na chenchi ya mafuta ikabaki.
Wewe ni mpenzi wa baiskeli? Upo tayari kumiliki baiskeli hii ya dhahabu?