Jeshi la Polisi latangaza nasafi za ajira

HomeKitaifa

Jeshi la Polisi latangaza nasafi za ajira

Jeshi la Polisi la Tanzania limetangaza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki, likiwataka kutuma maombi yao kupitia mfumo wa ajira wa jeshi hilo kabla ya tarehe 04 Aprili, 2025.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura Machi 20, 2025 nafasi hizo zinahusisha waombaji wenye elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na wahitimu wa shahada, stashahada na astashahada katika taaluma mbalimbali.

Miongoni mwa vigezo vilivyotajwa kwa waombaji ni kuwa na uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa, afya njema kimwili na kiakili iliyothibitishwa na daktari, kutokuwa na kumbukumbu za uhalifu, kutokuwa na alama za kuchorwa mwilini (tatoo), na kutowahi kutumia madawa ya kulevya ya aina yeyote.

Utaratibu wa kutuma Maombi

Waombaji wote wanatakiwa waandike barua za maombi yao kwa mkono bila kusahau namba za simu na watumie anuani ya Mkuu wa Jeshi la Polisi S.L.P 961 DODOMA. Barua hiyo inatakiwa kuambatanishwa kwenye maombi ikiwa kwenye mfumo wa ‘pdf.

Waombaji wote wanatakiwa wafanye maombi yao kupitia kwenye mfumo wa Ajira wa Polisi kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya www.ajira.tpf.go.tz huku nyaraka muhimu kama barua ya maombi, nakala za vyeti vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa, na kitambulisho cha utaifa (NIDA) zikiambatanishwa.

Jeshi hilo limeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa barua pepe, posta au kwa mkono hayatapokelewa, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa kwa wale watakaowasilisha nyaraka za kughushi au taarifa za uongo.

Hata hivyo, jeshi hilo halijabainisha idadi ya nafasi za ajira zilizotolewa kwa ajili ya vijana Wakitanzania.

error: Content is protected !!