Karani wa Sensa ya Watu na makazi Jiji la Arusha, Sarapia Kiwango, ameporwa kishikwambi chake, wakati akijiandaa kwenda kuhesabu makundi maalum, usiku wa kuamkia leo, huku mumewe akijeruhiwa.
Akizungumza na Daily News Digital, Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi katika Jiji la Arusha, Maneno Maziku, amesema, karani Kiwango aliporwa kishikwamb hicho na kwamba alipatiwa kingine kuendelea na kazi.
“Ni kweli aliporwa kishikwambi, huku mume wake akijeruhiwa kichwani, lakini ameshapewa kishikwambi kingine anaendelea na kazi, pia majeruhi hali yake inaendelea vizuri,” amesema.
Naye Diwani wa Kata ya Unga Limited, Mahamod Said na Mtendaji wa Kata hiyo, Sophia Laizer walizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti na kusema alivamiwa na watu waliokuwa na bodaboda.
“Jana usiku hawa makarani wa sensa waliitwa kwa mtendaji, wakati wanakwenda huko, ndiyo akakutana na vibaka waliokuwa kwenye bodaboda wakamjeruhi mumewe na kumpora kishikwambi, kisha kutoweka kusikojilikana,” amesema diwani huyo.