Katibu wa itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamidu Shaka, amewataja wanaohusika na upotevu wa zaidi ya Sh. Bilioni 2 kila mwezi katika ukusanyaji wa mapato mkoani Kigoma, wakiwamo wafanyabiashara na baadhi ya watumishi wa Serikali.
Shaka aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya Sekretarieti ya CCM wakifuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama katika Mkoa wa Kigoma waliotembelea bandari na reli.
alisema maeneo hayo ni sehemu ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ingawa bado hawajafanya vizuri, lipo eneo bado linalegalega.
“Nikupongeze Meneja mpya wa TRA, Gabriel Mwangosi, umekuja ni matumaini yangu kwamba utaanza na haya, nina taarifa kuwa umeanza vizuri hongera .. endelea kusimama vizuri unajua zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa mwezi zinapotea kwenye ukusanyaji wa ushuru wa forodha hili halipo sawa”, alisema Shaka.
Alisema “Mapato yanayokusanywa kwa mwezi kwa sasa ni shilingi 700 milioni lakini fedha hizo zinapotea katikati mjiulize zinakwenda wapi na kwanini haziingii katika mfumo wa Serikali.
“Wapo wafanyabiashara ambao wanajulikana, yupo ambaye kazi yake ni kuchezesha ili mapato ya katikati yanakwenda kwake na unao wafanyakazi ambao sio waaminifu wanashirikiana kuhujumu mapato ya serikali”.
Shaka ameongeza kwamba wapo wafanyabiashara wanaopiga dili na watumishi wa TRA, hivyo amemuelekeza meneja mpya kufuatilia kwa kina kwani wapo na wanawajua.