Lugha ya Kiswahili ni silaha ya taifa letu, imekuwa ya kwanza kutoka Bara la Afrika kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambayo inawazungumzaji wazungumzaji wengi zaidi ya milioni 200 duniani kote.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo Juni 6, 2022 wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Ni kwa kutambua umuhimu wa johari hii ya thamani na furaha yetu kwa mafanikio haya, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hii inaendelea na mikakati ya kuiongoza dunia kuadhimisha Siku hii kwa mara ya kwanza Julai 7, 2022 katika Balozi zetu kote Duniani, kama wasemavyo Waswahili “Hamadi ni ilio kibindoni, na silaha ni iliyo mkononi” Kiswahili ndiyo silaha yetu” amesema Waziri Mchengerwa.
Lugha adhimu ya Kiswahili imeendelea kukua na kuimarika na kukubalika kutumika kitaifa, kikanda na kimataifa hatua inayolitangaza vema taifa duniani.
“Naweza kujinasibu kuwa matumizi ya Kiswahili yanazidi kukubalika kitaifa, kikanda na kimataifa ambapo jitihada hizo kwa kipindi cha mwaka 2021/22 zimezaa matunda kwa Kiswahili kuvishwa joho jipya kuwa lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika” amesema Waziri Mchengerwa.
Pia ameliambia Bunge kuwa Kiswahili kimepitishwa kuwa lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Februari 5 – 6, 2022 Jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa hatua hiyo ni fursa muhimu kwa Wataalamu wa Tafsiri na Ukalimani nchini ambao katika muda mfupi, tayari Watanzania 65 wamesajiliwa kupata fursa za ajira za muda na za kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni zake.