Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki uzinduzi wa kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Ltd. tarehe 28 Juni 2025, jijini Dodoma pamoja Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Evariste Ndayishimiye.
Kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Limited kina uwezo wa kuzalisha tani milioni moja (1,000,000) kwa mwaka kwa kutumia mitambo 5 ya kisasa inayozalisha tani laki mbili (200,000) kila moja kwa mwaka.
Baadhi ya malighafi za samadi zinazozalishwa ni pamoja na mbolea asili kwa ajili ya kilimo hai, uchakataji wa mawe ya chokaa- kilimo, uchakataji wa madini ya fosifeti. Malighafi hizo huchanganywa na mbolea za kawaida za Urea, DAP na MOP ili kutengeneza mbolea za FOMI ambazo ni rafiki kwa udongo na mazingira.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Burundi na Serikali ya Tanzania wakiwemo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Gerald Mweli. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Menejimenti ya Wizara ya Kilimo na Wakuu wa Taasisi za Wizara.