Maagizo ya Rais Samia kuhusu marekebisho ya sheria

HomeKitaifa

Maagizo ya Rais Samia kuhusu marekebisho ya sheria

 Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Mipango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kufanya marekebisho ya sheria na mifumo ya  utoaji wa haki ili iweze kutatua migogoro kwa haraka.

Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Sheria yaliyofanyika jana Februari 1, 2023 katika viwanja vya Chinangali Dodoma amesema sheria na mifumo hiyo inayotumika kutatua migogoro ya uwekezaji inayotokea ikirekebishwa itakuwa kivutio kwa wafanyabiashara na wawekezaji wanaowekeza nchini.

“Hapana shaka hili litawavutia wawekezaji na wafanyabiashara kwani linalenga imani ya usalama wa mali zao,” amesema Rais Samia.

Mbali na kuimarisha sheria na mifumo ya utoaji haki, Rais Samia amesisitiza matumizi ya mbinu ya usuluhishi wa migogoro ya biashara na uwekezaji inayoibuka nchini ili kuokoa muda na fedha zinazotumika kuendesha kesi mahakamani.

“Ni vyema utaratibu wa usuluhishi upewe kipaumbele kutokana na faida zake kama zilivyoelezwa,” ameongeza Rais Samia.

Mbali na kuvutia wawekezaji mhimili wa mahakama unajukumu la kutoa hukumu na usuluhishi wa haki ili kuendeleza na kudumisha amani iliyopo nchini.

“Mara nyingi haki ikipotoea na amani inakuwa haipo. Kwa hiyo tujitahidi haki ipatikane ili amani iendelee kupatikana nchini.,” ameongeza kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Wala rushwa kukiona

Akihutubia kwenye maadhimisho hayo Rais Samia amewataka watumishi wanaochafua sura ya muhimili wa mahakama kwa kufanya vitendo viovu ikiwemo kutoa na kuchukua rushwa kuchukuliwa hatua kwa haraka.

“…wachulieni hatua wale watumishi ambao bado wanafanya vitendo viovu vya rushwa, kauli mbaya na unyanyasaji wa wanawake pamoja na watoto,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!