Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza mabalozi wa Tanzania nje ya nchi waimarishe biashara na nchi wanapokwenda kwani wana jukumu la kukuza uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya uchumi.
Ametoa maelekezo hayo jana ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma wakati alipokutana na mabalozi saba wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Sweden, Rwanda, India, Ethiopia, Uswisi na Jamhuri ya Korea.
“Waheshimiwa mabalozi mnajukumu kubwa la kukuza uchumi wetu. Nendeni mkaimarishe biashara yetu na nchi yetu. Muangalie sisi tumefanya nini na tumepungua wapi na je tunaweza kurekebisha vipi,” ameelekeza.
Pia ameongezea kwa kusema “Mmeshapata maelekezo kutoka kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hayo ndio maelekezo muhimu. Nendeni vituoni muda umeisha. Huu sio muda wa kwenda kuaga mawaziri. Wako wengi sana, naamini baada ya kuonana na viongozi wetu wakuu, sasa mko imara.”