Baada ya kulitumika jeshi kwa takribani miaka 43, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, amefunguka mambo kadha wa kadha kuhusu hali ya usalama wa nchi, mchango wa Tanzania katika kulinda amani wa nchi nyingine, changamoto alizopita na hapa uchangiaji wa jeshi kwenye uchumi wa nchi.
Mabeyo, aliyeanza kutumikia wadhifa huo mnamo Februari 6, 2017, baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, akichukua nafasi ya Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange, alieleza hayo wakati wa mahojiano maalum na kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV hapo Juni 22, 2022.
Hali ya usalama nchini
Mabeyo, ambaye aliagwa rasmi bungeni hapo Juni 14, 2022, huku Spika wa Bunge Tulia Ackson akimshukuru kwa “utumishi wako uliotukuka” ameweka wazi kwamba hali ya usalama nchi kwa sasa ni nzuri na kama taifa linaelekea pazuri kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tukampokea Rais mpya ambaye tunaendelea naye, mama Samia Suluhu Hassan na naamini kwamba tunaendelea vizuri nchi iko salama mpaka sasa wananchi wako watulivu wanaendelea kufuata miongozo kama inavyotolewa na serikali,”- CDF Mabeyo.
Matishio ya ugaidi
Mabeyo alitaja matishio ya ugaidi ambayo Tanzania imekuwa ikikabiliana nayo kwa miaka ya hivi karibuni kama moja ya “milima” aliyopaswa kuipanda wakati wa uongozi wake.
Matukio haya ni pamoja na yale ya Amboni, mkoani Tanga; Kibiti, mkoa wa Pwani; ugaidi huko mkoani Mwanza; na huko Mtwara kwenye mpaka na Msumbiji ambako magaidi wamekuwa wakifanya maisha ya jamii za karibu na mpaka huo kuwa magumu kwa kutokuwa na uhakika wa usalama wao.
“Kwa kweli, kipindi hicho kilikuwa kigumu sana lakini tunashukuru ushirikiano na wananchi, ushirikiano na vyombo vingine vya usalama, tumeweza kuhimili,” alibainisha Mabeyo kwenye mahojiano hayo.
“Lakini ni bahati mbaya kwamba majirani zetu [Msumbuji] wanakabiliwa sasa na tishio hilo [la ugaidi] kwa kiasi kikubwa. Na sisi kama sehemu ya ukanda wetu huu wa [Nchi za Kusini mwa Afrika] tumekubaliana kwamba tuwasaidie wenzetu,” aliongeza Mabeyo.
Aidha, Jenerali Mabeyo aliweka wazi kwa sasa hali ni nzuri hasa kwenye maeneo ambayo awali yaliathirika sana na matukio ya ugaidi kama Mtwara, Lindi, Tandahimba na Newala.
Uchangiaji wa jeshi kwenye uchumi wa nchi
Jenerali Mabeyo ameeleza kwamba kazi ya jeshi sio tu kulinda bali lina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi kupitia miradi mbalimbali iliyoanzishwa kama Shirika la Mzinga ambalo ni rasmi kuzalisha mazao ya jeshi.
“Shirika la SUMA, linajishughulisha katika kilimo na sasa hivi tuna kilimo kizuri cha umwagiliaji pale Chita, Morogoro, baada ya muda mfupi ujao Tanzania tutakuwa na akiba kubwa sana ya chakula, usalama wa chakula utakuwa ni mkubwa. Maana yake tutakuwa tunaongeza mapato ya serikali vilevile,”- Jenerali Mabeyo.
Aidha, Mabeyo alieleza ukiachilia mbali kilimo, jeshi pia linajenga na hivyo kupunguza matumizi ya serikali katika kuchukua wakandarasi wa nje na kuwalipa fedha nyingi huku akitolea mfano wa ujenzi wa Ikulu Dodoma.
Matamanio yake kwa jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema anatamani Jeshi letu liwe la kisasa zaidi na liweze kuchangia uchumi wa nchi na liwe la kujitegemea ‘sustainable military’.
“Kwa nini wenzetu wanatengeneza zana kutuuzia sisi, na kwa nini na sisi tusitengeneze zana za kututosheleza sisi wenyewe, wenzetu wana nyumba nzuri, hoteli, wanachangia uchumi wa nchi.
“Napenda Wanajeshi wote wawe na afya ya akili na wawe wanafikiria maendeleo muda wote,” anasema Mabeyo alipokuwa akihojiwa na ITV.
Hata hivyo, mkuu huyo wa majeshi alisema hali kwa sasa ni nzuri na hakuna changamoto ya kiusalama maeneo yoyote nchini kwani Jeshi linaendelea kushughulikia uwepo wa amani na kuhakikisha mipaka ipo salama.