Madhara 8 ya kuchora “Tattoo” mwilini.

HomeElimu

Madhara 8 ya kuchora “Tattoo” mwilini.

Tattoo ni sanaa ya kuchora kwa wino ngozi ya mwili wa binadamu ambayo kitaalamu huitwa “dermis” na huusisha kubadilisha rangi ya ngozi ambayo huweza kudumu kwa maisha yako yote au kwa muda tu kutegemea na aina na namna ya uwekaji.Dunia ya sasa kuchora “tattoo” ni kama “fasheni” na kuna uwezekano mkubwa sana “tattoo” iliyochorwa kwenye ngozi isitoke maisha yote hivyo kwa usalama ni vizuri kumuona mtaalamu wa “tattoo” ambaye ni mbobezi katika shughuli hiyo ingawa inaweza kuwa na gharama kubwa zaidi.Nchi ya Marekani ndiyo inaongoza duniani kote kwa kuwa na watu wengi wenye tattoo.
Kabla hujaamua kuchora tattoo ni vyema kutambua madhara yake kama ambavyo imeainishwa hapa chini.

1.Kansa ya Ngozi
Hapo mwanzoni wataalamu walikua wanasema hakuna mahusiano kati ya kansa ya ngozi na kuchora tattoo lakini hivi karibuni tafiti kutoka Uingereza zinaonyesha kuna aina fulani za wino ambazo zinaweza kusababisha kansa zikitumika kuchora tattoo.

2. Damu kuganda juu ya ngozi (Haematoma)
Hii husababishwa na kuvuja kwa damu nyingi chini ya ngozi, huonekana sana pembeni pembeni ya sehemu ambapo rangi ya tatoo imepita na huchelewa kupona kwa kidonda.

3. Mzio wa Ngozi (Allergy)
Haijalishi unaweka tattoo kwa muda au ya moja kwa moja, kumetokea kesi nyingi za watu wanaopata mzio wa ngozi baada ya kuchora tattoo. Utafiti unaonyesha rangi nyekundu ndio inaongoza kwa kusababisha mzio kuliko rangi nyingine kama nyeusi na purple. Mara nyingi “allergy” hizi huonekana mtu akikaa juani.

4. Makovu mwilini
Mwili unataambua tattoo kama adui wake hivyo hujaribu kuiondoa kwa njia mbalimbali na kwa kufanya hivyo husababisha makovu ya muda mrefu ambayo yanaweza kuleta magonjwa mengine ya ngozi.
5. Maambukizi ya UKIMWI na Ugonjwa wa Hepatitis B
Tabia ya kurudia sindano zilezile wakati wa kuchora tattoo kunaweza kusababisha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na maambukizi ya virusi vinavyoshambulia Ini (Hepatitis B). Ugonjwa wa Hepatitis B husababisha kansa ya Ini ambayo haitibiki. Ni vizuri kuwa makini ili uone kama sindano inayotumika kwako ni mpya.

6. Unaweza kukosa fursa mbalimbali
Kuna kampuni mbalimbali duniani haziwapi watu kazi kwa sababu tu wamechora tattoo kulingana na imani za kampuni husika. Lakini pia kazi ya Jeshi kwa baadhi ya nchi duniani haziruhusu tattoo hivyo kama wewe unayesoma hapa umeshachora tattoo ujue kazi ya jeshi kwa baadhi ya nchi huna tena.

7. Tattoo huingiliana na matumizi ya dawa fulani
Kama wewe unatumia dawa za kuzuia damu isigande mwilini ukichora tattoo inaweza kufanya utoke damu nyingi sana kwani dawa hizo huzuia uwezo wa mwili kukausha damu na kuponyesha vidonda.

8. Magonjwa ya ngozi
Wakati mwingine bacteria huweza kuvamia sehemu zenye vidonda vya tattoo na kusababisha kutopona haraka, dalili huweza kua homa kali, maumivu makali na sehemu ya tattoo kuvimba.

Aidha watalaamu wa hizi kazi wanasema ni ngumu sana kufuta tattoo japokuwa kuna kifaa kinachoitwa laser ambacho kinaweza kutumika kufuta tattoo yote au sehemu iliyochorwa tattoo. Japokuwa wanasema maumivu yanayotumiaka kufuta tattoo ni makali kuliko maumivu ya kuchora.

error: Content is protected !!