Mahakama Kuu ya Tanzania imetengua Kifungu cha 11 (1) (c) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 kinachozuia wafungwa kupiga kuira, kwa kusema kuwa kinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Elinaza Luvanda wakati mahakama hiyo ilipoketi Desemba 19 mwaka huu.
Uamuzi huo ulitokana na shauri lililofunguliwa na mwaharakati wa haki za binadamu Tito Magoti na wenzake, John Tulla, ambao wote walikosa haki ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa walikuwa mahabusu gerezani pamoja na kuwa walishajiandikisha kupiga kura.
Magoti na Tulla walifunguashauri hilo dhidi ya Tume ya Uchaguzi, (NEC), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Jeshi la Magereza.
Katika uamuzi huo, ilielezwa kwamba kifungu hicho kinakinzana na Ibara ya 5 (2) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoruhusu wafungwa na mahabusu kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu.
Jaji Luvanda alieleza kuwa kifungu hicho kiliandikwa kinyume cha watunga katiba.
“Kifungu hicho hakisemi kama ni kwa ajili ya wafungwa wa makosa ya jinai pekee au aina ya makosa isipokuwa kinasema wafungwa wa kuanzia miezi sita gerezani.
“Kutosema aina ya makosa yaliyomfanya mfungwa husika awepo gerezani, kinafanya kifungu hicho kiwe cha jumla, kwa maana kwamba kuna uwezekano wa mwananchi akafungwa kama mfungwa wa kesi ya madai ambaye naye ataingia katika mtego huo,” alisema Jaji Luvanda.