Wakati bomba la mafuta la Tanzania likitarajiwa kusafirisha dizeli kutoka Tanzania hadi Zambia, mawaziri wa sekta hizo wamekutana kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha ulinzi katika bomba hilo.
Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,710 sawa na maili 1,063, lilikuwa likisafirisha mafuta ghafi kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda eneo la Indeni Ndola, Zambia kwa ajili ya uchakataji.
Hata hivyo, serikali ya Zambia mapema mwaka huu ilisitisha uchakataji wa mafuta ghafi na ikaanza kuagiza moja kwa moja mafuta safi kutoka katika nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Kwa sasa bomba hilo ndilo litatumika kusafirisha dizeli kutoka Tanzania kwenda Zambia ambapo taratibu zote za mchakato huo zimeshafanyika.
Mawaziri hao ni January Makamba (Waziri wa Nishati, Tanzania), Mhandisi Peter Kapala (Waziri wa Nishati- Zambia), Ambrose Lufuma (Waziri wa Ulinzi- Zambia) pamoja na makatibu wa wizara hizo, waliokutana Dar es Salaam katika kikao cha siku mbili kujadili namna ya kuimarisha ulizni katika bomba hilo.