Majaliwa amwakilisha Rais kwenye mazishi ya Ole Nasha

HomeKitaifa

Majaliwa amwakilisha Rais kwenye mazishi ya Ole Nasha

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Samia Suluhu katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge Ngorongoro na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, William Tate Ole Nasha na amewasihi wananchi wamuenzi kwa kuyaendeleza mambo mazuri yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.

Majaliwa amesema kifo cha Ole Nasha ni pigo kubwa kwa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bunge pamoja na kwa wanafamilia na wananchi wa Ngorongoro.

Mazishi hayo ya Ole Nasha yamefanyika leo nyumbani kwake katika kijiji cha Osinoni, Kata ya Kakesyo wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha. Mbunge huyo alifariki Septemba 27, 2021 mkoani Dodoma.

Amesema jambo la muhimu kwa sasa ni kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. “Mke wa marehemu, watoto, ndugu, jamaa na wabunge nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Kwa upande wake, Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu –Uwekezaji, Geofrey Mwambe amesema Serikali hususani Ofisi ya Waziri Mkuu imepata pigo kubwa kwa kumpoteza mpiganaji kwa sababu marehemu Ole Nasha alikuwa mtumishi hodari.

error: Content is protected !!