Waziri wa Nishati, January Makamba ameeleza kiundani sababu za upandaji wa bei za mafuta baada ya kuwa na sintofahamu kutoka kwa wananchi waliokuwa wakihoji jambo hilo.
Waziri Makamba amesema chanzo kikubwa cha kupanda kwa bei za mafuta duniani ni vita kati ya Urusi na Ukraine na kueleza kwamba kikawaida nchi zinazozarisha mafuta duniani zikiingia kwenye mtafaluko lazima bei ya mafuta iyumbe.
“Tetesi tu kwamba kuna uwezekana wa kuwepo kwa vita inatosha kupandisha bei ya mafuta, na mtafahamu kwamba majeshi ya Urusi yalianza kuzingira mpaka wa Ukraine…vita imeanza tarehe 24 mwezi wa pili lakini nyuma ya hapo mapema mwezi wa kwanza tayari kulikua na tetesi ya kuwepo kwa vita,” amesema Waziri Makamba.
Alisema pia kuwa, baada ya tetesi hizo kuanza usambazaji wa mafuta ukasitishwa huku baadhi ya nchi zikiweka vikwaza kwa Urusi na mataifa kuacha kununua mafuta kutoka Urusi hivyo bei ikapanda.
Sababu ya pili, aliyoilezea Waziri Makamba ni kuhusu janga la Uviko-19 ulioanza mwezi Desemba 2019 na kusimamisha shughuli za uzalishaji wa vitu duniani pamoja na uzalishaji wa mafuta sababu watu walijifungia.
“Uviko-19 ulisimamisha uchumi wa dunia na shughuli za uzalishaji mali pamoja ikiwemo shughuli za uzalishaji wa mafuta kwenye visima. Kwahiyo kukatokea vitu viwili kwa mpigo, moja ni kwa sababu watu walijifungia hawakuwa wanafanya kazi, hawakuwa waasafiri kwahiyo uhitaji wa petroli ukashuka sana…mafuta yaliokuwa yanatumika wakati wa Covid ni yale yaliyokuwa kwenye mzunguko,” amesema Waziri Makamba.
Waziri Makamba amefafanua kwamba, baada ya hali ya maisha kurudi kama zamani kukawa na uhitaji mkubwa wa mafuta na hapo ndipo bei ikaanza kupanda sababu yaliyokuwepo hayakukidhi.
Aidha, Waziri Makamba ameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo kwamba ni, kutanua miundombinu ili kuleta meli kubwa zitakazo leta mafuta mengi zaidi, Kuboresha hifadhi ya mafuta TIPER ( Tanzania International Petroleum Reserves Limited) ili iwe na uwezo wa kuhifadhi mafuta mengi kwa wakati mmoja na kuboresha sehemu ya kushusha gesi ya kupikia LPG.