Mambo 6 muhimu unayopaswa kufahamu wakati unaanza chuo

HomeElimu

Mambo 6 muhimu unayopaswa kufahamu wakati unaanza chuo

 

Kutokana na furaha ya kufaulu na kwenda kusoma sehemu ambayo inakupa uhuru zaidi kwenye usomaji wako wanafunzi wengi wanakuwa na mitazamo tofauti kuhusu chuo, mazingira yae na namna watu wanavyoishi na hata namna ya kusoma. Wengi hutamani kujua mazingira na kila kitu kuhusu chuo. Hivi hapa ni baadhi ya vitu muhimu kuelewa kwa ujumla kabla hujaanza safari yako ya maisha ya chuo

 1.  Hautofundishwa kila kitu chuoni.
  Wanafunzi wa chuo wanaaminika kuwa ni watu wakubwa wenye uelewa na uwezo wa kutafuta maarifa zaidi hasa ukizingatia kuwa upatikanaji wa maarifa umekuwa mwepesi kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.  Wakufunzi hutumia mitaala kama miongozo tu ili kufundisha baadhi ya vitu na sehemu inayobakia mwanafunzi anajitafutia mwenyewe. Hili hufanyika ili kumjengea uwezo wa kujiamini, kuwasilisha na kuwasiliana.
 2. Ufaulu Mzuri
  Wengi wanapofika chuo hupokelewa na nadharia hasi kuwa hautaji ufaulu mkubwa ukiwa chuo kwani hamna ripoti inayotolewa wala hamna ushindani. Ukweli ni kwamba kuna faida nyingi za kuwa na ufaulu mzuri kwani itakupa nafasi nzuri ya kujiamini unapoomba ajira au mafunzo ya vitendo, na pia takusaidia kupata ufadhili wa masomo pale unapotaka kusoma zaidi.
 3. Tumia vipaji vyako
  Chuo ni sehemu inayokukutanisha na watu wengi na endapo utatumia vizuri kipaji chako itakupa nafasi na uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kwenye maisha yako. Maisha ya chuo ni fursa kwako kutumia kipaji ulichonacho nje ya taaluma unayopata. Pamoja na yote usisahau kuwa lengo kuu la wewe kuwa chuo ni kusoma na kupata maarifa.
 4. Uko karibu zaidi na tabia hatarishi
  Chuoni hamna bakora na muda mwingine haufuatiliwi kabisa ili kufahamu kama umeingia darasani au la. Unapokuwa chuo, wewe mwenyewe ndio msimamizi wa maisha yako. Uhuru unaongezeka wengi wanakuwa mbali na wazazi au walezi wao. Hivyo uhuru utakufanya utamani kujaribu kila kitu hata ambacho haujawahi kukifanya na ndipo wengi wanaishia kuwa walevi, wavutaji bangi au kuwa waasherati.
 5. Kuwa na watu
  Tambua kuwa kwa kiasi kikubwa, katika kila unachokifanya unategemea watu kufanikiwa. Ila unapaswa kuwa makini kuhakikisha watu unaowapata ni chanya na ambao watakusaidia kufikia malengo yako ndani na nje ya chuo. Ndani ya chuo watakusaidia kufanya kazi za darasani zitakazochochea ufaulu wako na watu wa nje mfano wenye taaluma inayofanana na wewe watakupa uzoefu kuhusiana na taaluma yako.
 6. Elimu haipimwi kwa mitihani
  Msemo huu haumaanishi kwamba utakapofanya vibaya pia utahitimu, hapana. Mitihani huja kukupima ili uweze kuhitimu lakini tambua elimu ya chuo ni pana inayohusisha pia mchango wa nini (wewe) unafanya nje ya darasa.

Kumbuka chuo ni sehemu bora zaidi ya kujifunza ambayo inakupa uwanja mpana kuelewa mambo na maisha pia

error: Content is protected !!