Mambo makubwa manne ya kujifunza Manara kutimkia Yanga

HomeMichezo

Mambo makubwa manne ya kujifunza Manara kutimkia Yanga

Katika hali isiyokuwa ya kawaida aliyekuwa Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara ametangazwa rasmi kujiunga na Klabu ya Yanga kama mhamasishaji. Hali hiyo imezua sintofahamu kwa mashabiki wa timu ya Simba kutokana na kitendo hicho kutokutegemewa kutokea hasa ukizingatia uhasama wa jadi uliopo kati ya miamba hii miwili ya soka nchini Tanzania.

Kitendo alichokifanya Manara kinachukuliwa kama kisasi na washabiki wa Yanga ambao walionekana kukwera sana na kitendo cha mshambuliaji machachari, Bernard Morisson kutimkia Simba mapema mwaka jana.

Kitendo cha Manara kuhamia Yanga tunakitazama kwa jicho la tofauti sana, kuna funzo/mafunzo ya kuchukua kwenye kitendo hicho. Wakati wengi bado wanajadili usaliti, unafiki, tamaa ya fedha juu ya Manara, lakini kuna mambo makubwa manne ya msingi ya kujifunza kwenye kitendo hicho (kutumia fursa, kujiamini, kujitambua pamoja na umuhimu wa kubobea kwenye fani fulani).

Kutumia Fursa – Haji anajua kutumia fursa vizuri. Hili ni zaidi ya kuwa Simba au Yanga, bali kujua wakati gani wa kuchukua hatua kwa manufaa binafsi. Haijalishi aliwahi kusema kitu gani dhidi ya Yanga huko nyuma, ila kila alichosema kiwe kibaya au kizuri, ilikuwa ni kulinda maslahi yake na maslahi ya klabu yake. Hii bado halimzuii Manara kufanya kazi Yanga, wala haitoi mapenzi yake kwa Simba, bali hili ni funzo kubwa sana. Unapofika wakati wa kufanya maamuzi magumu, ni vyema kutoruhusu hisia zikutawale, kwani zinaweza kufifisha uwezo wako wa kuamua kwa usahihi.

Kujiamini – Kujiamini ni silaha kubwa na muhimu sana maishani. Manara ameonesha kujiamini, amezungumza kile anachohisi ni sawa kwake bila woga. Akiwa amevalia jezi ya Yanga, amezungumza kana kwamba yumo ndani ya jezi ya Simba. Bashasha, hamasa na tamamshi yake yenye kujaa udhia mara nyingine yameendelea kutoka kama kawaida.

Kujitambua – Hapa ni kujua unataka nini na kwa wakati gani. Baada ya kuondoka Simba huenda hakuwa maalum ukiachilia mbali nafasi za ubalozi wa bidhaa mbalimbali alionao. Akiwa Simba amewahi kunukuliwa akisema, “Simba sio baba yangu wala mama yangu, hivyo siwezi kuacha mpunga (pesa) kisa tunafanya kazi Simba.”

Kubobea kwenye jambo fulani – Hakuna asiyejua kuwa Manara hana mapenzi na Yanga kama aliyokuwa nayo kwa Simba. Lakini unajua kwanini Yanga imeamua kumchukua Manara? Bila shaka ni kutokana na kipawa cha uhamasishaji alichonacho. Tukiondoa tofauti zilizopo kati ya wanachama wa Yanga na Manara, ni ukweli usiopingika kuwa kwenye suala la kutoa hamasa hana mpinzani kwa sasa.

Funzo la chukua hapa ni lipi? Ni kila mtu kuhakikisha kuwa ana jambo moja/mawili analoweza kufanya kwa ufasaha zaidi kuliko mtu mwingine. Hii itakusaidia kukupa fursa ya kufanya kazi katika mazingira yoyote kutokana tu na uwezo uliokua nao, sio tabia zako binafsi.

COMMENTS

error: Content is protected !!